Ufunuo 21:9-14
Ufunuo 21:9-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na yale mabakuli saba yaliyokuwa yamejaa mabaa saba ya mwisho, akaja na kuniambia, “Njoo! Nami nitakuonesha bibi arusi, mkewe Mwanakondoo!” Basi, Roho akanikumba, naye malaika akanipeleka juu ya mlima mrefu sana. Akanionesha mji mtakatifu, ukishuka kutoka kwa Mungu mbinguni, uking'aa kwa utukufu wa Mungu. Mwangaza wake ulikuwa kama wa jiwe la thamani kubwa kama yaspi, angavu kama kioo. Ulikuwa na ukuta mrefu na mkubwa, wenye milango kumi na miwili, na kila mmoja ulilindwa na malaika. Juu ya kila mlango paliandikwa mojawapo ya majina ya makabila kumi na mawili ya Israeli. Kila upande ulikuwa na milango mitatu: Upande wa mashariki milango mitatu, kaskazini milango mitatu, kusini milango mitatu na magharibi milango mitatu. Kuta za mji huo zilikuwa zimejengwa juu ya mawe ya msingi kumi na mawili, na juu ya kila jiwe palikuwa pameandikwa mojawapo ya majina ya wale mitume kumi na wawili wa Mwanakondoo.
Ufunuo 21:9-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akaja mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na vile vitasa saba vilivyojaa yale mapigo saba ya mwisho, naye akanena nami, akisema, Njoo huku, nami nitakuonyesha yule Bibi-arusi, mke wa Mwana-Kondoo. Akanichukua katika Roho mpaka mlima mkubwa, mrefu, akanionyesha ule mji mtakatifu, Yerusalemu, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mwenyezi Mungu; wenye utukufu wa Mungu, na mwangaza wake ulikuwa mfano wa kito chenye thamani nyingi kama kito cha yaspi, safi kama bilauri; ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu, wenye milango kumi na miwili, na katika ile milango malaika kumi na wawili; na majina yameandikwa ambayo ni majina ya kabila kumi na mbili za Waisraeli. Upande wa mashariki milango mitatu; na upande wa kaskazini milango mitatu; na upande wa kusini milango mitatu; na upande wa magharibi milango mitatu. Na ukuta wa mji ulikuwa na misingi kumi na miwili, na katika ile misingi majina kumi na mawili ya wale mitume kumi na wawili wa Mwana-Kondoo.
Ufunuo 21:9-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akaja mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na yale mabakuli saba yaliyojaa yale mapigo saba ya mwisho, naye akanena nami, akisema, Njoo huku, nami nitakuonesha yule Bibi arusi, mke wa Mwana-kondoo. Akanichukua katika Roho mpaka katika mlima mkubwa, mrefu, akanionesha ule mji mtakatifu, Yerusalemu, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mwenyezi Mungu; ukiwa na utukufu wa Mungu, na mwangaza wake ulikuwa mfano wa kito chenye thamani nyingi kama kito cha yaspi, safi kama bilauri; ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu, wenye milango kumi na miwili, na katika ile milango malaika kumi na wawili; na majina yameandikwa ambayo ni majina ya makabila kumi na mawili ya Waisraeli. Upande wa mashariki milango mitatu; na upande wa kaskazini milango mitatu; na upande wa kusini milango mitatu; na upande wa magharibi milango mitatu. Na ukuta wa mji ulikuwa na misingi kumi na miwili, na katika ile misingi kulikuwa na majina kumi na mawili ya wale mitume kumi na wawili wa Mwana-kondoo.
Ufunuo 21:9-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na yale mabakuli saba ya hayo mapigo saba ya mwisho akaja akaniambia, “Njoo, nami nitakuonyesha bibi arusi, yaani, mke wa Mwana-Kondoo.” Naye akanichukua katika Roho hadi kwenye mlima mkubwa na mrefu, akanionyesha ule Mji Mtakatifu, Yerusalemu, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu. Ulikuwa ukingʼaa kwa utukufu wa Mungu kama kito chenye thamani sana, kama yaspi, safi kama kioo. Ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu wenye malango kumi na mawili, pakiwa na malaika kumi na wawili kwenye hayo malango. Kwenye malango hayo yaliandikwa majina ya yale makabila kumi na mawili ya Israeli. Kulikuwa na malango matatu upande wa mashariki, matatu upande wa kaskazini, matatu upande wa kusini na matatu upande wa magharibi. Ukuta wa huo mji ulikuwa na misingi kumi na miwili, na juu yake yaliandikwa majina ya wale mitume kumi na wawili wa Mwana-Kondoo.