5
Kitabu na Mwana-Kondoo
1Kisha nikaona katika mkono wake wa kuume wa yule aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi, kitabu kilichoandikwa ndani na nje, kikiwa kimefungwa kwa mihuri saba. 2Nami nikamwona malaika mwenye nguvu akitangaza kwa sauti kuu, “Ni nani anayestahili kuivunja hiyo mihuri na kukifungua kitabu?” 3Lakini hapakuwa na yeyote mbinguni wala duniani au chini ya dunia aliyeweza kukifungua hicho kitabu, wala hata kutazama ndani yake. 4Nikalia sana kwa sababu hakuonekana yeyote anayestahili kukifungua hicho kitabu wala kutazama ndani yake. 5Kisha, mmoja wa wale wazee akaniambia, “Usilie! Tazama, Simba wa kabila la Yuda, wa Uzao wa Daudi, ameshinda. Yeye ndiye anayeweza kukifungua hicho kitabu na kuvunja mihuri yake saba.”
6Ndipo nikaona katikati ya kile kiti cha enzi na wale viumbe wenye uhai wanne, na katikati ya wale wazee, Mwana-Kondoo amesimama, akiwa kama amechinjwa. Alikuwa na pembe saba na macho saba, ambazo ndizo zile Roho saba#5:6 Roho saba za Mwenyezi Mungu hapa inamaanisha Roho wa Mungu katika ukamilifu wa utendaji wake. za Mungu zilizotumwa duniani pote. 7Huyo Mwana-Kondoo akaja na kukitwaa kile kitabu kutoka mkono wa kuume wa yule aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi. 8Alipokwisha kukitwaa kile kitabu, wale viumbe wenye uhai wanne pamoja na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele ya yule Mwana-Kondoo. Kila mmoja wao alikuwa na kinubi, nao walikuwa wameshika mabakuli ya dhahabu yaliyojaa uvumba, ambayo ni maombi ya watakatifu. 9Nao wakaimba wimbo mpya, wakisema:
“Wewe unastahili kukitwaa kitabu
na kuivunja mihuri yake,
kwa sababu ulichinjwa,
na kwa damu yako ukamnunulia Mungu
watu kutoka kila kabila, kila lugha,
kila jamaa na kila taifa.
10Wewe umewafanya hawa wawe ufalme na makuhani
wa kumtumikia Mungu wetu,
nao watatawala duniani.”
11Kisha nikatazama, nikasikia sauti za malaika wengi wakiwa wamekizunguka kile kiti cha enzi, pamoja na wale viumbe wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne. Idadi yao ilikuwa kumi elfu mara kumi elfu na maelfu ya maelfu. 12Nao waliimba kwa sauti kuu, wakisema:
“Anastahili Mwana-Kondoo, yeye aliyechinjwa,
kupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu
na heshima na utukufu na sifa!”
13Kisha nikasikia kila kiumbe mbinguni na duniani, chini ya nchi, na baharini, na vyote vilivyomo, vikiimba:
“Sifa na heshima na utukufu na uweza
ni vyake yeye aliyeketi juu ya hicho kiti cha enzi,
na kwa Mwana-Kondoo,
milele na milele!”
14Wale viumbe wenye uhai wanne wakasema, “Amen!” Nao wale wazee wakaanguka kifudifudi wakaabudu.