6
Mwana-Kondoo afungua mihuri saba
1Nikaangalia Mwana-Kondoo alipofungua ule muhuri wa kwanza miongoni mwa mihuri saba. Ndipo nikasikia mmoja wa wale viumbe wanne wenye uhai akisema kwa sauti kama ya radi: “Njoo!” 2Nikatazama, na hapo mbele yangu palikuwa na farasi mweupe! Yeye aliyempanda alikuwa na upinde, naye akapewa taji, akampanda akatoka akiwa kama mshindi aelekeaye katika kushinda.
3Alipouvunja ule muhuri wa pili, nikamsikia yule kiumbe wa pili mwenye uhai akisema, “Njoo!” 4Ndipo akatokea farasi mwingine mwekundu sana. Yeye aliyempanda akapewa uwezo wa kuondoa amani duniani na kuwafanya watu wauane. Yeye akapewa upanga mkubwa.
5Mwana-kondoo alipouvunja ule muhuri wa tatu, nikamsikia yule kiumbe wa tatu mwenye uhai akisema, “Njoo!” Nikatazama, na mbele yangu palikuwa na farasi mweusi! Yeye aliyempanda alikuwa na mizani mkononi mwake. 6Ndipo nikasikia kile kilichokuwa kama sauti katikati ya wale viumbe wanne wenye uhai ikisema, “Kipimo kimoja#6:6 Ni kama lita moja. cha ngano kwa mshahara wa kibarua wa siku moja#6:6 Sawa na dinari moja., na vipimo vitatu vya shayiri kwa mshahara wa kibarua cha siku moja. Lakini usiharibu mafuta wala divai!”
7Alipouvunja ule muhuri wa nne, nikasikia sauti ya yule kiumbe wa nne mwenye uhai ikisema, “Njoo!” 8Nikatazama, na hapo mbele yangu palikuwa na farasi mwenye rangi ya kijivujivu! Yeye aliyempanda aliitwa Mauti, naye Kuzimu#6:8 Kuzimu kwa Kiyunani ni Hades, yaani mahali pa wafu. alikuwa akimfuata nyuma yake kwa karibu. Wakapewa mamlaka juu ya robo ya dunia, kuua kwa upanga, njaa, tauni na kwa wanyama wakali wa dunia.
9Mwana-kondoo alipouvunja ule muhuri wa tano, nikaona chini ya madhabahu, roho za wale waliochinjwa kwa ajili ya neno la Mungu na kwa ajili ya ushuhuda walioutunza. 10Wakalia kwa sauti kuu, wakasema, “Hata lini, Ee Bwana Mungu Mwenyezi, uliye mtakatifu na mwaminifu, hutawahukumu na kulipiza kisasi kwa watu wanaoishi duniani kwa ajili ya damu yetu?” 11Kisha kila mmoja wao akapewa joho jeupe na wakaambiwa wangoje kwa muda kidogo zaidi, hadi idadi ya ndugu zao na watumishi wenzao watakaouawa kama wao walivyouawa, itakapotimia.
12Nikatazama alipouvunja ule muhuri wa sita. Pakatokea tetemeko kuu la ardhi, na jua likawa jeusi kama gunia lililotengenezwa kwa singa za mbuzi, na mwezi wote ukawa mwekundu kama damu. 13Nyota zilizo angani zikaanguka ardhini kama vile matunda ya mtini yasiyokomaa yaangukavyo wakati mti wake unapotikiswa na upepo mkali. 14Anga ikatoweka kama vile karatasi isokotwavyo, na kila mlima na kila kisiwa kikaondolewa mahali pake.
15Ndipo wafalme wa dunia, wakuu wote, majemadari, matajiri, wenye nguvu na kila mtu, mtumwa na mtu huru, wakajificha katika mapango na kwenye miamba ya milima. 16Wakaiita milima na miamba wakisema, “Tuangukieni, mkatufiche na uso wake yeye aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi, na mkatuepushe na ghadhabu ya Mwana-Kondoo! 17Kwa maana siku ile kuu ya ghadhabu yao imewadia. Je, ni nani awezaye kustahimili?”