Ufunuo 7
7
Waisraeli 144,000 watiwa muhuri
1Baada ya hili nikaona malaika wanne wakiwa wamesimama katika pembe nne za dunia, wakizuia hizo pepo nne za dunia, ili pasiwe na upepo utakaovuma juu ya nchi au juu ya bahari au juu ya mti wowote. 2Nikaona malaika mwingine akipanda kutoka mawio ya jua akiwa na muhuri wa Mungu aliye hai. Akawaita kwa sauti kubwa wale malaika wanne waliokuwa wamepewa mamlaka ya kuidhuru nchi na bahari, akisema, 3“Msiidhuru nchi wala bahari, wala miti, hadi tuwe tumetia muhuri kwenye paji za nyuso za watumishi wa Mungu wetu.” 4Ndipo nikasikia idadi ya wale waliotiwa muhuri: elfu mia moja na arobaini na nne kutoka makabila yote ya Israeli.
5Kutoka kabila la Yuda elfu kumi na mbili walitiwa muhuri,
kutoka kabila la Reubeni elfu kumi na mbili,
kutoka kabila la Gadi elfu kumi na mbili,
6kutoka kabila la Asheri elfu kumi na mbili,
kutoka kabila la Naftali elfu kumi na mbili,
kutoka kabila la Manase elfu kumi na mbili,
7kutoka kabila la Simeoni elfu kumi na mbili,
kutoka kabila la Lawi elfu kumi na mbili,
kutoka kabila la Isakari elfu kumi na mbili,
8kutoka kabila la Zabuloni elfu kumi na mbili,
kutoka kabila la Yusufu elfu kumi na mbili,
na kutoka kabila la Benyamini elfu kumi na mbili.
Umati mkubwa wa watu kutoka mataifa yote
9Baada ya hili nikatazama na hapo mbele yangu palikuwa na umati mkubwa wa watu ambao hakuna yeyote awezaye kuwahesabu, kutoka kila taifa, kila kabila, kila jamaa na kila lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi na mbele ya Mwana-Kondoo. Walikuwa wamevaa mavazi meupe na wakiwa wameshika matawi ya mitende mikononi mwao. 10Nao walikuwa wakipaza sauti kwa nguvu, wakisema:
“Wokovu una Mungu wetu,
yeye aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi,
na Mwana-Kondoo!”
11Malaika wote walikuwa wamesimama kukizunguka kile kiti cha enzi na wale wazee, na wale viumbe wanne wenye uhai. Wakaanguka kifudifudi mbele ya hicho kiti cha enzi na kumwabudu Mungu, 12wakisema:
“Amen!
Sifa na utukufu
na hekima na shukrani na heshima
na uweza na nguvu
viwe kwa Mungu wetu milele na milele.
Amen!”
13Kisha mmoja wa wale wazee akaniuliza, “Ni nani hawa waliovaa mavazi meupe, nao wametoka wapi?”
14Nikamjibu, “Bwana, wewe unajua.”
Naye akasema, “Hawa ni wale waliotoka katika ile dhiki kuu, nao wamefua mavazi yao katika damu ya Mwana-Kondoo na kuyafanya meupe kabisa. 15Kwa hiyo,
“Wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu
na kumtumikia usiku na mchana
katika Hekalu lake;
naye aliyeketi katika kile kiti cha enzi
atatanda hema lake juu yao.
16Kamwe hawataona njaa
wala kiu tena.
Jua halitawachoma
wala joto lolote liunguzalo.#7:16 Isaya 49:10
17Kwa maana Mwana-Kondoo
aliyeko katikati ya kile kiti cha enzi
atakuwa Mchungaji wao;
naye atawaongoza kwenda
kwenye chemchemi za maji yaliyo hai#7:17 Isaya 49:10.
Naye Mungu atawafuta machozi
kutoka machoni mwao#7:17 Isaya 25:8.”
Iliyochaguliwa sasa
Ufunuo 7: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.