Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ufunuo 9:13-21

Ufunuo 9:13-21 NEN

Malaika wa sita akaipiga tarumbeta yake, nami nikasikia sauti ikitoka katika zile pembe za madhabahu ya dhahabu iliyoko mbele za Mungu. Ile sauti ikamwambia yule malaika wa sita mwenye tarumbeta, “Wafungulie wale malaika wanne waliofungwa kwenye ule mto mkubwa Frati.” Basi wale malaika wanne, waliokuwa wamewekwa tayari kwa ajili ya saa hiyo, na siku hiyo, na mwezi huo, na mwaka huo ili wawaue theluthi ya wanadamu wakafunguliwa. Idadi ya majeshi wapanda farasi ilikuwa 200,000,000. Nilisikia idadi yao. Hivi ndivyo nilivyowaona hao farasi na wapanda farasi katika maono yangu: Wapanda farasi walivaa dirii vifuani zenye rangi nyekundu sana kama ya moto na yakuti samawi na kiberiti. Vichwa vya hao farasi vilikuwa kama vichwa vya simba, na moto, moshi na kiberiti vilitoka vinywani mwao. Theluthi ya wanadamu wakauawa kwa mapigo hayo matatu, yaani, huo moto, moshi na kiberiti, vilivyotoka kwenye vinywa vya hao farasi. Nguvu za hao farasi zilikuwa katika vinywa vyao na kwenye mikia yao, kwa sababu mikia yao ilikuwa kama nyoka, yenye vichwa ambayo waliitumia kudhuru. Wanadamu waliosalia, ambao hawakuuawa katika mapigo hayo, bado walikataa kutubia kazi za mikono yao na hawakuacha kuabudu mashetani na sanamu za dhahabu, za fedha, za shaba, za mawe na za miti, ambazo haziwezi kuona, kusikia wala kutembea. Wala hawakutubu na kuacha matendo yao ya uuaji, uchawi, uasherati wala wizi wao.