Ufunuo 9:13-21
Ufunuo 9:13-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha, malaika wa sita akapiga tarumbeta yake. Nami nikasikia sauti moja kutoka katika pembe nne za madhabahu ya dhahabu iliyokuwa mbele ya Mungu. Sauti hiyo ikamwambia huyo malaika wa sita mwenye tarumbeta, “Wafungulie malaika wanne waliofungwa kwenye mto mkubwa Eufrate!” Naye akawafungulia malaika hao wanne ambao walikuwa wametayarishwa kwa ajili ya saa hiyo ya siku ya mwezi huo wa mwaka huohuo, kuua theluthi moja ya wanadamu. Nilisikia idadi ya majeshi wapandafarasi ilikuwa 200,000,000. Hivi ndivyo nilivyowaona hao farasi na wapandafarasi katika hiyo njozi: Walikuwa na ngao vifuani zilizokuwa moto mtupu, zenye rangi ya samawati na manjano kama madini ya kiberiti. Vichwa vya hao farasi vilikuwa kama vya simba; na moto, moshi, na madini ya kiberiti vilikuwa vinatoka vinywani mwao. Theluthi moja ya wanadamu waliuawa kwa mabaa hayo matatu, yaani moto, moshi na madini ya kiberiti, yaliyokuwa yanatoka katika vinywa vyao; maana nguvu ya farasi hao ilikuwa vinywani mwao na katika mikia yao. Mikia yao ilifanana na nyoka na ilikuwa na vichwa, nao waliitumia hiyo kuwadhuru watu. Wanadamu wengine waliobaki ambao hawakuuawa na mabaa hayo, hawakutubu na kuviacha vitu walivyokuwa wametengeneza kwa mikono yao wenyewe; wala kuacha kuabudu pepo, sanamu za dhahabu, fedha, shaba, mawe na miti, vitu ambavyo haviwezi kuona, kusikia wala kutembea. Wala hawakutubu na kuacha kufanya mauaji, uchawi, uzinzi, na wizi.
Ufunuo 9:13-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Malaika wa sita akapiga baragumu, nikasikia sauti moja iliyotoka katika zile pembe za madhabahu ya dhahabu iliyo mbele za Mungu, ikimwambia yule malaika wa sita aliyekuwa na baragumu, Wafungue nao malaika wanne waliofungwa kwenye mto mkubwa Frati. Wale malaika wanne wakafunguliwa, waliokuwa wamewekwa tayari kwa ile saa na siku na mwezi na mwaka, ili kwamba waue theluthi ya wanadamu. Na hesabu ya majeshi ya wapanda farasi ilikuwa milioni mia mbili; nilisikia hesabu yao. Hivyo ndivyo nilivyowaona hao farasi katika maono yangu, nao waliokaa juu yao, wana dirii kifuani, za wekundu kama wa moto, na buluu kama johari ya rangi ya samawati na manjano kama kiberiti, na vichwa vya farasi hao ni kama vichwa vya simba, na katika vinywa vyao hutoka moto na moshi na kiberiti. Theluthi ya wanadamu wakauawa kwa mapigo matatu hayo, kwa moto huo na moshi huo na kiberiti hicho, yaliyotoka katika vinywa vyao. Kwa maana nguvu za hao farasi ni katika vinywa vyao, na katika mikia yao; maana mikia yao ni mfano wa nyoka, ina vichwa, nao wanadhuru kwavyo. Na wanadamu waliobakia, wasiouawa kwa mapigo hayo, hawakuzitubia zile kazi za mikono yao, hata wasiwasujudie mashetani, na sanamu za dhahabu na za fedha na za shaba na za mawe na za miti, zisizoweza kuona wala kusikia wala kutembea. Wala hawakuutubia uuaji wao, wala uchawi wao, wala uasherati wao, wala wizi wao.
Ufunuo 9:13-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Malaika wa sita akapiga baragumu, nikasikia sauti moja iliyotoka katika zile pembe za madhabahu ya dhahabu iliyo mbele za Mungu, ikimwambia yule malaika wa sita aliyekuwa na baragumu, Wafungue nao malaika wanne waliofungwa kwenye mto mkubwa Frati. Wale malaika wanne wakafunguliwa, waliokuwa wamewekwa tayari kwa ile saa na siku na mwezi na mwaka, ili kwamba waue theluthi ya wanadamu. Na hesabu ya majeshi ya wapanda farasi ilikuwa elfu ishirini mara elfu kumi; nilisikia hesabu yao. Hiyo ndivyo nilivyowaona hao farasi katika maono yangu, nao waliokaa juu yao, wana dirii kifuani, kama za moto, na za samawi, na za kiberiti; na vichwa vya farasi hao ni kama vichwa vya simba, na katika vinywa vyao hutoka moto na moshi na kiberiti. Theluthi ya wanadamu wakauawa kwa mapigo matatu hayo, kwa moto huo na moshi huo na kiberiti hicho, yaliyotoka katika vinywa vyao. Kwa maana nguvu za hao farasi ni katika vinywa vyao, na katika mikia yao; maana mikia yao ni mfano wa nyoka, ina vichwa, nao wanadhuru kwa hivyo. Na wanadamu waliosalia, wasiouawa kwa mapigo hayo, hawakuzitubia zile kazi za mikono yao, hata wasiwasujudie mashetani, na sanamu za dhahabu na za fedha na za shaba na za mawe na za miti, zisizoweza kuona wala kusikia wala kuenenda. Wala hawakuutubia uuaji wao, wala uchawi wao, wala uasherati wao, wala wivi wao.
Ufunuo 9:13-21 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Malaika wa sita akaipiga tarumbeta yake, nami nikasikia sauti ikitoka katika zile pembe za madhabahu ya dhahabu iliyoko mbele za Mungu. Ile sauti ikamwambia yule malaika wa sita mwenye tarumbeta, “Wafungulie wale malaika wanne waliofungwa kwenye ule mto mkubwa Frati.” Basi wale malaika wanne, waliokuwa wamewekwa tayari kwa ajili ya saa hiyo, na siku hiyo, na mwezi huo, na mwaka huo ili wawaue theluthi ya wanadamu wakafunguliwa. Idadi ya majeshi wapanda farasi ilikuwa 200,000,000. Nilisikia idadi yao. Hivi ndivyo nilivyowaona hao farasi na wapanda farasi katika maono yangu: Wapanda farasi walivaa dirii vifuani zenye rangi nyekundu sana kama ya moto na yakuti samawi na kiberiti. Vichwa vya hao farasi vilikuwa kama vichwa vya simba, na moto, moshi na kiberiti vilitoka vinywani mwao. Theluthi ya wanadamu wakauawa kwa mapigo hayo matatu, yaani, huo moto, moshi na kiberiti, vilivyotoka kwenye vinywa vya hao farasi. Nguvu za hao farasi zilikuwa katika vinywa vyao na kwenye mikia yao, kwa sababu mikia yao ilikuwa kama nyoka, yenye vichwa ambayo waliitumia kudhuru. Wanadamu waliosalia, ambao hawakuuawa katika mapigo hayo, bado walikataa kutubia kazi za mikono yao na hawakuacha kuabudu mashetani na sanamu za dhahabu, za fedha, za shaba, za mawe na za miti, ambazo haziwezi kuona, kusikia wala kutembea. Wala hawakutubu na kuacha matendo yao ya uuaji, uchawi, uasherati wala wizi wao.