Warumi 3:9-20
Warumi 3:9-20 NEN
Tusemeje basi? Je, sisi ni bora kuwaliko wao? La hasha! Kwa maana tumekwisha kuhakikisha kwa vyovyote kwamba Wayahudi na watu wa Mataifa wote wako chini ya nguvu ya dhambi. Kama ilivyoandikwa: “Hakuna mwenye haki, hakuna hata mmoja. Hakuna hata mmoja mwenye ufahamu, hakuna hata mmoja amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wote wameoza pamoja; hakuna atendaye mema, naam, hakuna hata mmoja.” “Makoo yao ni makaburi wazi; kwa ndimi zao wao hufanya udanganyifu.” “Sumu ya nyoka iko midomoni mwao.” “Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu.” “Miguu yao ina haraka kumwaga damu; maangamizi na taabu viko katika njia zao, wala njia ya amani hawaijui.” “Hakuna hofu ya Mungu machoni pao.” Basi tunajua ya kwamba chochote sheria inachosema, inawaambia wale walio chini ya sheria ili kila kinywa kinyamazishwe na ulimwengu wote uwajibike kwa Mungu. Kwa hiyo hakuna binadamu hata mmoja atakayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa matendo ya sheria, kwa maana sheria hutufanya tuitambue dhambi.