Warumi 4:16-25
Warumi 4:16-25 NENO
Kwa hiyo, ahadi huja kupitia kwa imani, ili iwe ni kwa neema, na ihakikishiwe wazao wote wa Ibrahimu, si kwa wale walio wa sheria peke yao, bali pia kwa wale walio wa imani ya Ibrahimu. Yeye ndiye baba yetu sisi sote. Kama ilivyoandikwa: “Nimekufanya wewe kuwa baba wa mataifa mengi.” Yeye ni baba yetu mbele za Mungu, ambaye yeye alimwamini, yule Mungu anayefufua waliokufa, na kuvitaja vitu ambavyo haviko kana kwamba viko. Akitarajia yasiyoweza kutarajiwa, Ibrahimu akaamini, akawa baba wa mataifa mengi, kama alivyoahidiwa kwamba, “Hivyo ndivyo uzao wako utakavyokuwa.” Ibrahimu hakuwa dhaifu katika imani hata alipofikiri hali ya mwili wake, ambao ulikuwa kama uliokufa, kwani umri wake ulikuwa unakaribia miaka mia moja, au alipofikiri hali ya kufa ya tumbo la Sara. Lakini Ibrahimu hakusitasita kwa kutokuamini ahadi ya Mungu, bali alitiwa nguvu katika imani yake na kumpa Mungu utukufu, akiwa na hakika kabisa kwamba Mungu alikuwa na uwezo wa kutimiza lile aliloahidi. Hii ndio sababu, “ilihesabiwa kwake kuwa haki.” Maneno haya “ilihesabiwa kwake kuwa haki,” hayakuandikwa kwa ajili yake peke yake, bali kwa ajili yetu sisi pia ambao Mungu atatupatia haki, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Isa Bwana wetu kutoka kwa wafu. Alitolewa afe kwa ajili ya dhambi zetu, naye alifufuliwa kutoka mauti ili tuhesabiwe haki.