Warumi 9:22-33
Warumi 9:22-33 NEN
Iweje basi, kama Mungu kwa kutaka kuonyesha ghadhabu yake na kufanya uweza wake ujulikane, amevumilia kwa uvumilivu mwingi vile vyombo vya ghadhabu vilivyoandaliwa kwa uharibifu? Iweje basi, kama yeye alitenda hivi ili kufanya wingi wa utukufu wake ujulikane kwa vile vyombo vya rehema yake, alivyotangulia kuvitengeneza kwa ajili ya utukufu wake, yaani pamoja na sisi, ambao pia alituita, si kutoka kwa Wayahudi peke yao, bali pia kutoka kwa watu wa Mataifa? Kama vile Mungu asemavyo katika Hosea: “Nitawaita ‘watu wangu’ wale ambao si watu wangu; nami nitamwita ‘mpenzi wangu’ yeye ambaye si mpenzi wangu,” tena, “Itakuwa hasa mahali pale walipoambiwa, ‘Ninyi si watu wangu,’ wao wataitwa ‘wana wa Mungu aliye hai.’ ” Isaya anapiga kelele kuhusu Israeli: “Ingawa idadi ya wana wa Israeli ni wengi kama mchanga wa pwani, ni mabaki yao tu watakaookolewa. Kwa kuwa Bwana ataitekeleza hukumu yake duniani kwa haraka na kwa ukamilifu.” Ni kama vile alivyotabiri Isaya akisema: “Kama Bwana Mwenye Nguvu Zote asingelituachia uzao, tungelikuwa kama Sodoma, tungelifanana na Gomora.” Kwa hiyo tuseme nini basi? Kwamba watu wa Mataifa ambao hawakutafuta haki, wamepata haki ile iliyo kwa njia ya imani. Lakini Israeli, ambao walijitahidi kupata haki kwa njia ya sheria, hawakuipata. Kwa nini? Kwa sababu hawakuitafuta kwa njia ya imani bali kwa njia ya matendo. Wakajikwaa kwenye lile “jiwe la kukwaza.” Kama ilivyoandikwa: “Tazama naweka katika Sayuni jiwe la kukwaza watu na mwamba wa kuwaangusha. Yeyote atakayemwamini hataaibika kamwe.”