Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Wimbo 5

5
Mpenzi
1Nimekuja kwenye bustani yangu, dada yangu,
bibi arusi wangu;
nimekusanya manemane yangu pamoja
na manukato yangu.
Nimekula sega langu la asali na asali yangu;
nimekunywa divai yangu na maziwa yangu.
Rafiki
Kuleni, enyi rafiki, mnywe;
kunyweni ya kutosha, ee wapenzi.
Mpendwa
2Nililala lakini moyo wangu ulikuwa macho.
Sikiliza! Mpenzi wangu anabisha:
“Nifungulie, dada yangu, mpendwa wangu,
hua wangu, usiye na hitilafu.
Kichwa changu kimeloa umande,
na nywele zangu manyunyu ya usiku.”
3Nimevua joho langu:
je, ni lazima nivae tena?
Nimenawa miguu yangu:
je, ni lazima niichafue tena?
4Mpenzi wangu aliweka mkono wake kwenye tundu la komeo;
moyo wangu ulianza kugonga kwa ajili yake.
5Niliinuka kumfungulia mpenzi wangu,
mikono yangu ikidondosha manemane,
vidole vyangu vikitiririka manemane,
penye vipini vya komeo.
6Nilimfungulia mpenzi wangu,
lakini mpenzi wangu alishaondoka;
alikuwa ameenda zake.
Moyo wangu ulishuka kwa kuondoka kwake.
Nilimtafuta lakini sikumpata.
Nilimwita lakini hakunijibu.
7Walinzi walinikuta
walipokuwa wakifanya zamu za ulinzi mjini.
Walinipiga, wakanijeruhi,
wakaninyang’anya joho langu,
hao walinzi wa kuta!
8Enyi binti za Yerusalemu, ninawaagiza:
mkimpata mpenzi wangu,
mtamwambia nini?
Mwambieni ninazimia kwa mapenzi.
Rafiki
9Je, mpenzi wako ni bora kuliko wengine namna gani,
wewe uliye mzuri kupita wanawake wote?
Je, mpenzi wako ni mzuri kuliko wengine, namna gani,
hata unatuagiza hivyo?
Mpendwa
10Mpenzi wangu anang’aa, tena ni mwekundu,
wa kuvutia miongoni mwa wanaume kumi elfu.
11Kichwa chake ni dhahabu safi kuliko zote,
nywele zake ni za mawimbi
na ni nyeusi kama kunguru.
12Macho yake ni kama ya hua
kandokando ya vijito vya maji,
aliyeogeshwa kwenye maziwa,
yaliyopangwa kama vito vya thamani.
13Mashavu yake ni kama matuta
ya mimea ya manukato.
Midomo yake ni kama yungiyungi
inayodondosha manemane.
14Mikono yake ni fimbo za dhahabu
iliyopambwa kwa krisolitho.
Mwili wake ni kama pembe ya ndovu iliyong’arishwa
iliyopambwa na yakuti samawi.
15Miguu yake ni nguzo za marumaru
zilizosimikwa katika vitako vya dhahabu safi.
Sura yake ni kama Lebanoni,
bora kama miti yake ya mierezi.
16Kinywa chake chenyewe ni utamu,
kwa ujumla yeye ni wa kupendeza.
Huyu ndiye mpenzi wangu, huyu ndiye rafiki yangu,
ee binti za Yerusalemu.

Iliyochaguliwa sasa

Wimbo 5: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia