Tito 3
3
Maagizo mbalimbali
1Wakumbushe watu kunyenyekea kwa watawala na kwa wenye mamlaka, na kutii, wakiwa tayari kutenda kila lililo jema, 2wasimnenee mtu yeyote mabaya, wasiwe wagomvi bali wawe wema, wakiwa wapole kwa watu wote.
3Maana sisi wenyewe wakati fulani tulikuwa wajinga, wasiotii, tukiwa watumwa wa tamaa mbaya na anasa za kila aina. Tuliishi katika uovu na wivu, tukichukiwa na kuchukiana sisi kwa sisi. 4Lakini wema na upendo wa Mungu Mwokozi wetu ulipofunuliwa, 5alituokoa, si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyotenda, bali kwa sababu ya rehema zake. Alituokoa kwa kutuosha kwa kuzaliwa mara ya pili na kwa kufanywa wapya kupitia kwa Roho Mtakatifu wa Mungu, 6ambaye Mungu alitumiminia kwa wingi kupitia kwa Isa Al-Masihi Mwokozi wetu, 7ili, tukiisha kuhesabiwa haki kwa neema yake, tupate kuwa warithi tukiwa na tumaini la uzima wa milele. 8Hili ni neno la kuaminiwa. Nami nataka uyasisitize mambo haya, ili wale ambao wamemwamini Mungu wapate kuwa waangalifu kujitoa kwa ajili ya kutenda mema wakati wote. Mambo haya ni mazuri tena ya manufaa kwa kila mtu.
9Lakini jiepushe na maswali ya kipuzi, mambo ya koo, mabishano na ugomvi kuhusu sheria, kwa sababu hayana faida, tena ni ubatili. 10Mtu anayesababisha mafarakano, mwonye mara ya kwanza, kisha mwonye mara ya pili. Baada ya hapo, usihusike naye tena. 11Kwa kuwa unajua kwamba mtu kama huyo amepotoka na tena ni mwenye dhambi. Yeye amejihukumu mwenyewe.
Maneno ya mwisho
12Mara nitakapomtuma Artema au Tikiko kwako, jitahidi kuja unione huko Nikopoli, kwa sababu nimeamua kukaa huko wakati wa majira ya baridi. 13Fanya kila uwezalo uwasafirishe Zena yule mwanasheria na Apolo na uhakikishe kwamba wana kila kitu wanachohitaji katika safari yao.
14Watu wetu hawana budi kujifunza kutenda mema, ili waweze kuyakimu mahitaji ya kila siku, wasije wakaishi maisha yasiyokuwa na matunda.
15Wote walio pamoja nami wanakusalimu.
Wasalimu wale wanaotupenda katika imani.
Neema iwe nanyi nyote. Amen.
Iliyochaguliwa sasa
Tito 3: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.