1 Fal 13:11-22
1 Fal 13:11-22 SUV
Basi nabii mmoja mzee alikuwa akikaa katika Betheli; na wanawe wakamwendea wakamwambia kila neno alilolitenda yule mtu wa Mungu siku ile katika Betheli; na maneno aliyomwambia mfalme, hayo nayo walimwambia baba yao. Baba yao akawaambia, Amekwenda zake kwa njia ipi? Kwa maana wanawe walikuwa wameiona njia ile aliyoiendea yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda. Akawaambia wanawe, Nitandikieni punda. Wakamtandikia punda, naye akampanda. Akamfuata mtu wa Mungu, akamkuta ameketi chini ya mwaloni, akamwambia, Je! Wewe ndiwe yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda? Akamwambia, Mimi ndiye. Akamwambia, Karibu kwangu nyumbani, ule chakula. Naye akamwambia, Siwezi kurudi pamoja nawe, wala kuingia pamoja nawe; wala sili chakula wala sinywi maji pamoja nawe hapa; kwani nimeambiwa kwa neno la BWANA, Usile chakula wala usinywe maji huko, wala usirudi kwa njia ile uliyoijia. Akamwambia, Mimi nami ni nabii kama wewe, na malaika akaniambia kwa neno la BWANA, kusema, Mrudishe pamoja nawe nyumbani kwako, ale chakula, akanywe maji. Lakini alisema uongo. Basi mtu yule akarudi pamoja naye, akala chakula, akanywa maji nyumbani mwake. Hata ikawa, walipokuwa wameketi mezani, neno la BWANA likamjia nabii yule aliyemrudisha; akamlilia yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda, akinena, BWANA asema hivi, Kwa sababu umeiasi kauli ya BWANA, wala hukuishika amri ile aliyokuamuru BWANA, Mungu wako, bali umerudi, ukala chakula ukanywa maji, hapo alipokuambia, Usile chakula, wala usinywe maji; maiti yako haitaliingia kaburi la baba zako.