Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Fal 8:54-66

1 Fal 8:54-66 SUV

Hata ikawa, Sulemani alipokwisha kumwomba BWANA maombi hayo, na dua hiyo yote, akasimama na kuondoka hapo mbele ya madhabahu ya BWANA, hapo alipokuwa amepiga magoti, na kuikunjua mikono yake kuelekea mbinguni. Akasimama, na kuwabariki mkutano wote wa Israeli kwa sauti kuu, akasema, Na ahimidiwe BWANA, aliyewapa watu wake Israeli kustarehe, vile vile kama yote aliyoyaahidi. Halikukosa kupatikana neno lo lote katika ahadi yake njema, aliyoahidi kwa mkono wa Musa, mtumishi wake. BWANA, Mungu wetu, na akae nasi, kama alivyokaa na baba zetu; asituache, wala asitutupe; aielekeze mioyo yetu kwake, ili tuende katika njia zake zote, na kuzishika amri zake, na sheria zake, na hukumu zake, alizowaamuru baba zetu. Na maneno yangu haya, niliyoyaomba mbele za BWANA, na yawe karibu na BWANA, Mungu wetu, mchana na usiku, ili aitetee haki ya mtumishi wake, na haki ya watu wake Israeli, kwa kadiri ya haja zao za kila siku. Watu wote wa ulimwengu wajue ya kuwa BWANA ndiye Mungu; hakuna mwingine. Mioyo yenu na iwe kamili kwa BWANA, Mungu wetu, kuenenda katika sheria zake, na kuzishika amri zake, kama ilivyo leo. Ndipo mfalme, na Israeli wote pamoja naye, wakatoa sadaka mbele za BWANA. Sulemani akatoa sadaka za amani, alizomtolea BWANA, ng’ombe ishirini na mbili elfu, na kondoo mia na ishirini elfu. Ndivyo mfalme na wana wa Israeli wote walivyoifanya wakfu nyumba ya BWANA. Siku ile ile mfalme akaitakasa behewa ya katikati iliyokuwa mbele ya nyumba ya BWANA; kwa kuwa hapo ndipo alipotoa sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya unga, na mafuta ya sadaka za amani; kwa sababu ile madhabahu ya shaba iliyokuwa mbele za BWANA ilikuwa ndogo, haikutosha kuzipokea sadaka za kuteketezwa, na sadaka za unga, na mafuta ya sadaka za amani. Basi, wakati ule Sulemani akafanya sikukuu, na Israeli wote pamoja naye, kusanyiko kubwa sana, kutoka maingilio ya Hamathi mpaka kijito cha Misri, mbele za BWANA, Mungu wetu, siku saba na siku saba, yaani siku kumi na nne. Hata siku ya nane akaagana na watu, nao wakambarikia mfalme, wakaenda hemani kwao, wakifurahi na kuchangamka moyoni kwa wema wote BWANA aliomfanyia Daudi mtumishi wake, na Israeli watu wake.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 1 Fal 8:54-66