Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 8:54-66

1 Wafalme 8:54-66 Biblia Habari Njema (BHN)

Solomoni alipomaliza kusema sala hiyo yote na ombi lake kwa Mwenyezi-Mungu aliinuka kutoka pale mbele ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu, mahali alipokuwa amepiga magoti akiinua mikono yake juu. Alisimama, akawabariki Waisraeli wote waliokuwa wamekusanyika hapo, akisema kwa sauti kubwa, “Atukuzwe Mwenyezi-Mungu ambaye amewapatia starehe watu wake Israeli, kulingana na ahadi yake. Ametimiza ahadi zake zote njema alizozitoa kupitia kwa mtumishi wake Mose. Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, awe nasi, kama alivyokuwa na babu zetu; tunaomba asituache, wala asitutupe. Yeye aelekeze mioyo yetu kwake, ili tufuate njia zake, tukishika amri zake, maongozi yake na maagizo yake aliyowapa babu zetu. Basi, maneno yangu haya ambayo ni ombi langu mbele ya Mwenyezi-Mungu, yawe karibu na Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, mchana na usiku, naye amjalie mtumishi wake, na watu wake Israeli, ili wafanikiwe katika haja zao za kila siku. Nayo mataifa yote ulimwenguni yatajua kwamba kweli Mwenyezi-Mungu ndiye Mungu; wala hakuna mwingine. Nanyi, muwe waaminifu kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, mkifuata masharti yake na kutii amri zake zote kama mnavyofanya hivi leo.” Kisha, mfalme Solomoni na Waisraeli wote waliokuwa pamoja naye walimtolea Mwenyezi-Mungu tambiko. Naye Solomoni alimtolea Mwenyezi-Mungu tambiko za amani: Ng'ombe 22,000 na kondoo 120,000. Hivyo ndivyo mfalme na watu wote wa Israeli walivyoiweka wakfu nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Siku hiyohiyo, mfalme aliiweka wakfu sehemu ya katikati ya ua uliokuwa mbele ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu kwani hapo ndipo alipotolea sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka, na mafuta ya sadaka za amani; kwa sababu ile madhabahu ya shaba haikutosha sadaka hizo zote. Naye Solomoni kwa muda wa siku saba na siku saba zaidi, yaani kwa siku kumi na nne, alifanya sikukuu pamoja na Waisraeli wote; nao walitoka tangu kiingilio cha Hamathi, hadi mto wa Misri. Katika siku ya nane, Solomoni aliwaaga watu; nao wakamtakia baraka mfalme, wakaenda kwao wakishangilia na kufurahi kwa sababu ya wema ambao Mwenyezi-Mungu aliuonesha kwa Daudi, mtumishi wake, na kwa watu wake Israeli

1 Wafalme 8:54-66 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Hata ikawa, Sulemani alipokwisha kumwomba BWANA maombi hayo, na dua hiyo yote, akasimama na kuondoka hapo mbele ya madhabahu ya BWANA, hapo alipokuwa amepiga magoti, na kuikunjua mikono yake kuelekea mbinguni. Akasimama, na kuwabariki mkutano wote wa Israeli kwa sauti kuu, akasema, Na ahimidiwe BWANA, aliyewapa watu wake Israeli kustarehe, vile vile kama yote aliyoyaahidi. Halikukosa kupatikana neno lolote katika ahadi yake njema, aliyoahidi kwa mkono wa Musa, mtumishi wake. BWANA, Mungu wetu, na akae nasi, kama alivyokaa na baba zetu; asituache, wala asitutupe; aielekeze mioyo yetu kwake, ili tuende katika njia zake zote, na kuzishika amri zake, na sheria zake, na hukumu zake, alizowaamuru baba zetu. Na maneno yangu haya, niliyoyaomba mbele za BWANA, na yawe karibu na BWANA, Mungu wetu, mchana na usiku, ili aitetee haki ya mtumishi wake, na haki ya watu wake Israeli, kwa kadiri ya haja zao za kila siku. Watu wote wa ulimwengu wajue ya kuwa BWANA ndiye Mungu; hakuna mwingine. Mioyo yenu na iwe kamili kwa BWANA, Mungu wetu, kuenenda katika sheria zake, na kuzishika amri zake, kama ilivyo leo. Ndipo mfalme, na Israeli wote pamoja naye, wakatoa sadaka mbele za BWANA. Sulemani akatoa sadaka za amani, alizomtolea BWANA, ng'ombe elfu ishirini na mbili, na kondoo elfu mia moja na ishirini. Ndivyo mfalme na wana wa Israeli wote walivyoiweka wakfu nyumba ya BWANA. Siku ile ile mfalme akaitakasa behewa ya katikati iliyokuwa mbele ya nyumba ya BWANA; kwa kuwa hapo ndipo alipotoa sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya unga, na mafuta ya sadaka za amani; kwa sababu ile madhabahu ya shaba iliyokuwa mbele za BWANA ilikuwa ndogo, haikutosha kuzipokea sadaka za kuteketezwa, na sadaka za unga, na mafuta ya sadaka za amani. Basi, wakati ule Sulemani akafanya sikukuu, na Israeli wote pamoja naye, kusanyiko kubwa sana, kutoka maingilio ya Hamathi mpaka kijito cha Misri, mbele za BWANA, Mungu wetu, siku saba na siku saba, yaani siku kumi na nne. Hata siku ya nane akaagana na watu, nao wakambarikia mfalme, wakaenda hemani kwao, wakifurahi na kuchangamka moyoni kwa wema wote BWANA aliomfanyia Daudi mtumishi wake, na Israeli watu wake.

1 Wafalme 8:54-66 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Hata ikawa, Sulemani alipokwisha kumwomba BWANA maombi hayo, na dua hiyo yote, akasimama na kuondoka hapo mbele ya madhabahu ya BWANA, hapo alipokuwa amepiga magoti, na kuikunjua mikono yake kuelekea mbinguni. Akasimama, na kuwabariki mkutano wote wa Israeli kwa sauti kuu, akasema, Na ahimidiwe BWANA, aliyewapa watu wake Israeli kustarehe, vile vile kama yote aliyoyaahidi. Halikukosa kupatikana neno lo lote katika ahadi yake njema, aliyoahidi kwa mkono wa Musa, mtumishi wake. BWANA, Mungu wetu, na akae nasi, kama alivyokaa na baba zetu; asituache, wala asitutupe; aielekeze mioyo yetu kwake, ili tuende katika njia zake zote, na kuzishika amri zake, na sheria zake, na hukumu zake, alizowaamuru baba zetu. Na maneno yangu haya, niliyoyaomba mbele za BWANA, na yawe karibu na BWANA, Mungu wetu, mchana na usiku, ili aitetee haki ya mtumishi wake, na haki ya watu wake Israeli, kwa kadiri ya haja zao za kila siku. Watu wote wa ulimwengu wajue ya kuwa BWANA ndiye Mungu; hakuna mwingine. Mioyo yenu na iwe kamili kwa BWANA, Mungu wetu, kuenenda katika sheria zake, na kuzishika amri zake, kama ilivyo leo. Ndipo mfalme, na Israeli wote pamoja naye, wakatoa sadaka mbele za BWANA. Sulemani akatoa sadaka za amani, alizomtolea BWANA, ng’ombe ishirini na mbili elfu, na kondoo mia na ishirini elfu. Ndivyo mfalme na wana wa Israeli wote walivyoifanya wakfu nyumba ya BWANA. Siku ile ile mfalme akaitakasa behewa ya katikati iliyokuwa mbele ya nyumba ya BWANA; kwa kuwa hapo ndipo alipotoa sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya unga, na mafuta ya sadaka za amani; kwa sababu ile madhabahu ya shaba iliyokuwa mbele za BWANA ilikuwa ndogo, haikutosha kuzipokea sadaka za kuteketezwa, na sadaka za unga, na mafuta ya sadaka za amani. Basi, wakati ule Sulemani akafanya sikukuu, na Israeli wote pamoja naye, kusanyiko kubwa sana, kutoka maingilio ya Hamathi mpaka kijito cha Misri, mbele za BWANA, Mungu wetu, siku saba na siku saba, yaani siku kumi na nne. Hata siku ya nane akaagana na watu, nao wakambarikia mfalme, wakaenda hemani kwao, wakifurahi na kuchangamka moyoni kwa wema wote BWANA aliomfanyia Daudi mtumishi wake, na Israeli watu wake.

1 Wafalme 8:54-66 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Wakati Solomoni alipomaliza dua hizi zote na maombi kwa BWANA, akainuka kutoka mbele ya madhabahu ya BWANA, mahali alipokuwa amepiga magoti, mikono yake ikawa imekunjuliwa kuelekea juu mbinguni. Akasimama na kubariki kusanyiko lote la Israeli kwa sauti kubwa akisema: “Ahimidiwe BWANA, aliyewapa pumziko watu wake Israeli kama vile alivyokuwa ameahidi. Hakuna hata neno moja lililopunguka kati ya ahadi zote nzuri alizozitoa kupitia mtumishi wake Mose. BWANA Mungu wetu na awe pamoja nasi kama alivyokuwa na baba zetu, kamwe asituache wala kutukataa. Yeye na aielekeze mioyo yetu kwake, ili tutembee katika njia zake zote na kuzishika amri na maagizo na masharti aliyowapa baba zetu. Nami maneno yangu haya, ambayo nimeyaomba mbele za BWANA, yawe karibu na BWANA Mungu wetu usiku na mchana, ili kwamba atetee shauri la mtumishi wake na la watu wake Israeli kulingana na hitaji lao la kila siku, ili kwamba mataifa yote ya dunia wajue kwamba BWANA ndiye Mungu na kwamba hakuna mwingine. Lakini ni lazima mwiweke mioyo yenu kikamilifu kwa BWANA Mungu wetu, kuishi kwa maagizo yake na kutii amri zake, kama ilivyo wakati huu.” Kisha mfalme na Israeli wote pamoja naye wakatoa dhabihu mbele za BWANA. Solomoni akatoa dhabihu sadaka za amani kwa BWANA: ngʼombe 22,000, pamoja na kondoo na mbuzi 120,000. Hivyo ndivyo mfalme na Waisraeli wote walivyoweka wakfu Hekalu la BWANA. Siku iyo hiyo mfalme akaweka wakfu sehemu ya katikati ya ua uliokuwa mbele ya Hekalu la BWANA na hapo akatoa sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka na mafuta ya sadaka za amani, kwa sababu madhabahu ya shaba iliyokuwa mbele za BWANA ilikuwa ndogo sana kuweza kubeba sadaka hizo za kuteketezwa, sadaka za nafaka na mafuta ya sadaka ya amani. Hivyo Solomoni akaiadhimisha sikukuu kwa wakati ule, na Israeli wote pamoja naye. Walikuwa kusanyiko kubwa sana, watu kutoka Lebo-Hamathi hadi Kijito cha Misri. Wakaiadhimisha mbele za BWANA Mungu wetu kwa siku saba na siku saba zaidi, yaani, jumla siku kumi na nne. Siku iliyofuata, aliwaruhusu watu waondoke. Wakambariki mfalme, kisha wakaenda nyumbani, wakiwa na mashangilio na furaha rohoni kwa ajili ya mambo yote mema ambayo BWANA ametenda kwa ajili ya Daudi mtumishi wake na watu wake Israeli.