2 Kor 6:11-18
2 Kor 6:11-18 SUV
Vinywa vyetu vimefumbuliwa kwenu, enyi Wakorintho; mioyo yetu imekunjuliwa. Hamsongwi ndani yetu, bali mwasongwa katika mioyo yenu. Basi, ili mlipe kadiri ile mliyopewa (nasema nanyi kama na watoto), nanyi pia mkunjuliwe mioyo. Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini? Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha. Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike, asema Bwana Mwenyezi.