Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Fal 13:1-13

2 Fal 13:1-13 SUV

Katika mwaka wa ishirini na tatu wa Yoashi mwana wa Ahazia, mfalme wa Yuda, Yehoahazi mwana wa Yehu alianza kutawala juu ya Israeli katika Samaria; akatawala miaka kumi na saba. Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, akayafuata makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli; wala hakuyaacha. Hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, akawatia mkononi mwa Hazaeli mfalme wa Shamu, na mkononi mwa Ben-hadadi mwana wa Hazaeli, siku zote. Naye Yehoahazi akamsihi BWANA, BWANA akamsikiliza; kwa kuwa aliyaona mateso ya Israeli, jinsi mfalme wa Shamu alivyowatesa. (BWANA akawapa Israeli mwokozi, nao wakatoka mikononi mwa Washami; wana wa Israeli wakakaa hemani mwao kama zamani za kwanza. Lakini hawakuyaacha makosa ya nyumba ya Yeroboamu, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli, lakini wakaendelea katika hayo; nayo ile Ashera ikakaa vivyo katika Samaria). Kwa kuwa hakumwachia Yehoahazi watu ila wapandao farasi hamsini, na magari kumi, na askari elfu kumi waendao kwa miguu; kwa kuwa mfalme wa Shamu aliwaharibu, akawaponda mfano wa mavumbi yaliyokanyagwa. Basi mambo yote ya Yehoahazi yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na ushujaa wake, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli? Yehoahazi akalala na babaze; wakamzika katika Samaria. Na Yehoashi mwanawe akatawala mahali pake. Katika mwaka wa thelathini na saba wa Yoashi mfalme wa Yuda, Yehoashi mwana wa Yehoahazi alianza kutawala juu ya Israeli katika Samaria, akatawala miaka kumi na sita. Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA; hakuyaacha makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli; lakini akaendelea katika hayo. Basi mambo yote ya Yehoashi yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na ushujaa wake aliopigania na Amazia mfalme wa Yuda, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli? Yehoashi akalala na babaze; na Yeroboamu akakaa katika kiti chake cha enzi; naye Yehoashi akazikwa huko Samaria, pamoja na wafalme wa Israeli.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 2 Fal 13:1-13