2 Sam 18
18
Kushindwa na Kuuawa kwa Absalomu
1Kisha Daudi akawahesabu watu waliokuwa pamoja naye, akaweka maakida wa elfu elfu, na maakida wa mia mia juu yao. 2#2 Sam 15:19Daudi akawapeleka hao watu vitani, theluthi moja chini ya mkono wa Yoabu, na theluthi ya pili chini ya mkono wa Abishai, mwana wa Seruya nduguye Yoabu, na theluthi ya tatu chini ya mkono wa Itai, Mgiti. Mfalme akawaambia watu, Bila shaka mimi mwenyewe nami nitatoka pamoja nanyi. 3#2 Sam 21:17Lakini watu wakasema, Wewe usitoke nje; kwa maana tukikimbia, hawatatuona sisi kuwa kitu; au tukifa nusu yetu, hawatatuona kuwa kitu; lakini wewe u wa thamani kuliko watu elfu kumi katika sisi; kwa hivyo sasa ni afadhali ukae tayari kutusaidia toka mjini. 4Mfalme akawaambia, Yaliyo mema machoni penu ndiyo nitakayofanya. Basi mfalme akasimama kando ya lango, na hao watu wakatoka kwa elfu zao na mia zao. 5Mfalme akawaamuru Yoabu na Abishai na Itai, akasema, Mtendeeni yule kijana, Absalomu, kwa upole kwa ajili yangu. Nao watu wote wakasikia, mfalme alipowaagiza maakida wote katika habari za Absalomu. 6#Yos 17:15,18Hivyo watu wakatoka waende nyikani ili kupigana na Israeli; na vita vikatokea ndani ya msitu wa Efraimu. 7#Mit 11:21Watu wa Israeli wakapigwa huko mbele ya watumishi wa Daudi, kukawa na maangamizo makuu huko siku ile, ya watu ishirini elfu. 8Kwa maana vita vilienea huko juu ya uso wote wa nchi; na siku ile huo msitu ukala watu wengi kuliko wale walioliwa na upanga. 9#2 Sam 14:26; 17:23; Ayu 18:5-14; Mt 27:5; 1 Kor 11:14Na kwa bahati Absalomu akakutana na watumishi wa Daudi. Naye Absalomu alikuwa amepanda nyumbu wake, na yule nyumbu akapita chini ya matawi manene ya mwaloni mkubwa, hata kichwa chake kikakwama katika mwaloni huo, akanyakuliwa juu kati ya mbingu na nchi; na yule nyumbu aliyekuwa chini yake akaenda mbele. 10Basi mtu mmoja akaona hayo, akaenda akamwambia Yoabu, akasema, Tazama, mimi nalimwona Absalomu ametundikwa katika mwaloni. 11Naye Yoabu akamwambia mtu yule aliyempasha habari, Je! Wewe umeona haya; Mbona, basi, hukumpiga hata nchi papo hapo? Nami ningalikupa fedha kumi na mshipi. 12Yule mtu akamwambia Yoabu, Kama ningalipata fedha elfu mkononi mwangu, hata hivyo singalinyosha mkono wangu juu ya mwana wa mfalme; kwa maana mfalme masikioni mwetu alikuagiza wewe, na Abishai na Itai, akisema, Angalieni sana mtu awaye yote asimguse yule kijana, Absalomu. 13Na tena, kama ningaliitendea roho yake kwa hila; (wala hapana neno lo lote liwezalo kufichwa mbele ya mfalme); ndipo wewe mwenyewe ungalijitenga. 14Ndipo Yoabu akasema, Siwezi kungoja na kusema nawe hivi. Akachukua vyemba vitatu mkononi mwake, akamchoma Absalomu moyoni, alipokuwa akali hai katikati ya ule mwaloni. 15Kisha vijana kumi, waliomchukulia Yoabu silaha zake wakamzunguka, wakampiga Absalomu, na kumwua.
16Kisha Yoabu akapiga tarumbeta, wakarudi watu toka kuwafuatia Israeli; kwani Yoabu akawazuia watu. 17#Yos 7:26; 8:29; Yer 22:18,19; Omb 3:53Nao wakamtwaa Absalomu wakamtupa katika shimo kubwa mle msituni, wakaweka juu yake chungu kubwa sana la mawe; kisha Israeli wote wakakimbia kila mtu hemani mwake. 18#Mwa 14:17; 2 Sam 14:27; Ayu 13:12; 18:17,19; Zab 34:16; 109:13; Mit 2:22; Zab 49:11Huyo Absalomu alipokuwa yu hai alikuwa ameitwaa na kujiinulia ile nguzo iliyoko bondeni mwa mfalme; kwa maana alisema, Mimi sina mtoto wa kulikumbusha jina langu; akaiita hiyo nguzo kwa jina lake mwenyewe nayo inaitwa ziara la Absalomu hata hivi leo.
Daudi Asikia kuhusu Kifo cha Absalomu
19 #
2 Sam 15:36; 17:17 Basi Ahimaasi, mwana wa Sadoki, akasema, Niende mbio sasa, nikampelekee mfalme habari, jinsi BWANA alivyomlipiza kisasi juu ya adui zake. 20Yoabu akamwambia, Wewe hutakuwa mchukua habari leo, siku nyingine utachukua habari; lakini leo hutachukua habari, kwa sababu mwana wa mfalme amekufa. 21Ndipo Yoabu akamwambia Mkushi mmoja, Nenda ukamwambie mfalme hayo uliyoyaona. Na huyo Mkushi akajiinamisha mbele ya Yoabu, akaenda zake mbio. 22Ndipo Ahimaasi, mwana wa Sadoki, akamwambia Yoabu mara ya pili, Haidhuru, tafadhali nipe ruhusa, nipige mbio na mimi nyuma ya huyo Mkushi. Naye Yoabu akasema, Mbona wewe unataka kupiga mbio, mwanangu, kwa maana hutapata kitu kwa habari hizo unazopeleka? 23Akasema, Haidhuru, nitapiga mbio. Akamwambia, Haya, piga mbio. Ndipo Ahimaasi akapiga mbio, akishika njia ya uwandani, akampita yule Mkushi.
24 #
1 Sam 1:9; 4:13; 2 Sam 13:34; 2 Fal 9:17; Isa 31:6-9 Basi Daudi alikuwa ameketi kati ya malango mawili; mlinzi akapanda juu hata dari ya lile lango hata ukutani, akainua macho yake, akaangalia, na tazama, mtu anakuja mbio peke yake. 25Mlinzi akalia, akamwambia mfalme. Naye mfalme akasema, Kama yu peke yake, ana habari kinywani mwake. Akaja mbio, akakaribia. 26Kisha huyo mlinzi akaona mtu mwingine anapiga mbio; mlinzi akamwita bawabu, akasema, Angalia, mtu mwingine anakuja mbio peke yake. Mfalme akasema, Huyu naye analeta habari. 27#1 Fal 1:42Na huyo mlinzi akasema, Nionavyo mimi, kupiga mbio kwake yule wa kwanza ni kama kupiga mbio kwake Ahimaasi, mwana wa Sadoki. Naye mfalme akasema, Yeye ni mtu mwema, anakuja na habari njema. 28Ahimaasi akainua sauti yake, akamwambia mfalme, Amani. Akainama mbele ya mfalme kifudifudi, akasema, Ahimidiwe BWANA, Mungu wako, aliyewatoa watu hao walioiinua mikono yao juu ya bwana wangu, mfalme. 29Mfalme akauliza, Je! Yule kijana, Absalomu, yu salama? Ahimaasi akajibu, Yoabu aliponituma mimi mtumishi wa mfalme, mimi mtumishi wako, naliona kishindo kikubwa, lakini sikujua sababu yake. 30Naye mfalme akasema, Geuka, usimame hapa. Akageuka, akasimama. 31#Zab 27:2; 55:18Na tazama, yule Mkushi akafika; Mkushi akasema, Nina habari kwa bwana wangu mfalme; kwa maana BWANA amekulipizia kisasi leo juu ya hao wote walioinuka kupigana nawe. 32Naye mfalme akamwambia yule Mkushi, Yule kijana, Absalomu, je! Yu salama? Yule Mkushi akajibu, Adui za bwana wangu mfalme, na wote wainukao ili kukudhuru, na wawe kama alivyo yule kijana.
Daudi Amwombolezea Absalomu
33 #
2 Sam 19:4; Mit 10:1; 19:13 Naye mfalme akataabika sana, akapanda juu, akaingia kile chumba kilichokuwa juu ya lango, akalia; na katika kwenda kwake alisema hivi, Mwanangu Absalomu! Ee mwanangu! Mwanangu Absalomu! Laiti ningalikufa badala yako, Absalomu, mwanangu, mwanangu!
Iliyochaguliwa sasa
2 Sam 18: SUV
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.