Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mdo 13:1-12

Mdo 13:1-12 SUV

Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao. Basi watu hao, wakiisha kupelekwa na Roho Mtakatifu wakatelemkia Seleukia, na kutoka huko wakasafiri baharini hata Kipro. Na walipokuwa katika Salami wakalihubiri neno la Mungu katika masinagogi ya Wayahudi, nao walikuwa naye Yohana kuwa mtumishi wao. Walipokwisha kupita katikati ya kisiwa chote mpaka Pafo, wakaona mtu mmoja, mchawi, nabii wa uongo, Myahudi jina lake Bar-Yesu; mtu huyu alikuwa pamoja na liwali Sergio Paulo, mtu mwenye akili. Yeye liwali akawaita Barnaba na Sauli waje kwake, akataka kulisikia neno la Mungu. Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake), akashindana nao, akitaka kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani. Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho, akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka? Basi, angalia, mkono wa Bwana u juu yako, nawe utakuwa kipofu, usilione jua kwa muda. Mara kiwi kikamwangukia na giza, akazunguka-zunguka na kumtafuta mtu wa kumshika mkono na kumwongoza. Ndipo yule liwali, alipoyaona yaliyotendeka, akaamini, akiyastaajabia mafundisho ya Bwana.