Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mdo 27:21-44

Mdo 27:21-44 SUV

Na walipokuwa wamekaa wakati mwingi bila kula chakula, Paulo akasimama katikati yao, akasema, Wanaume, iliwapasa kunisikiliza mimi na kutokung’oa nanga huko Krete, na kupata madhara haya na hasara hii. Sasa nawapeni shauri, iweni na moyo mkuu, kwa maana hapana hata nafsi mmoja miongoni mwenu atakayepotea, ila merikebu tu. Kwa maana usiku huu wa leo malaika wa Mungu yule ambaye mimi ni wake, naye ndiye nimwabuduye, alisimama karibu nami, akaniambia, Usiogope, Paulo, huna budi kusimama mbele ya Kaisari; tena, tazama, Mungu amekupa watu wote wanaosafiri pamoja nawe. Basi, wanaume, changamkeni; kwa sababu namwamini Mungu, ya kwamba yatakuwa vile vile kama nilivyoambiwa. Lakini hatuna budi kupwelewa katika kisiwa kimoja. Hata usiku wa kumi na nne ulipofika, tulipokuwa tukichukuliwa huko na huko katika bahari ya Adria, kama usiku wa manane baharia wakadhani ya kuwa wanaikaribia nchi kavu. Wakatupa bildi wakapata pima ishirini, wakaendelea kidogo wakatupa bildi tena, wakapata pima kumi na tano. Wakachelea tusije tukapwelewa mahali penye miamba, wakatupa nanga nne za tezi, wakaomba kuche. Na baharia walipotaka kukimbia na kuiacha merikebu, wakiishusha mashua baharini kana kwamba wanataka kutupa nanga za omo, Paulo akawaambia akida na askari, Hawa wasipokaa ndani ya merikebu hamtaweza kuokoka. Basi askari wakazikata kamba za mashua, wakaiacha ianguke. Na kulipokuwa kukipambauka Paulo akawasihi wote wale chakula, akisema, Leo ni siku ya kumi na nne kungoja na kufunga, hamkula kitu cho chote. Basi nawasihi mle chakula, maana itakuwa kwa wokovu wenu; kwa maana hapana hata unywele wa kichwa cha mmoja wenu utakaopotea. Alipokwisha kusema hayo akatwaa mkate, akamshukuru Mungu mbele yao wote akaumega akaanza kula. Ndipo wakachangamka wote, wakala chakula wenyewe. Na sisi tuliokuwa ndani ya merikebu tulipata watu mia mbili na sabini na sita. Walipokwisha kushiba wakaipunguza shehena ya merikebu, wakiitupa ngano baharini. Kulipokucha hawakuitambua ile nchi, ila waliona hori yenye ufuo, wakashauriana kuiegesha merikebu huko, kama ikiwezekana. Wakazitupilia mbali zile nanga, na kuziacha baharini, pamoja na kuzilegeza kamba za sukani, wakalitweka tanga dogo ili liushike upepo, wakauendea ule ufuo. Lakini wakafikia mahali palipokutana bahari mbili, wakaiegesha merikebu, omo ikakwama ikakaa isitikiswe, bali tezi ilikuwa imefumuliwa kwa nguvu za mawimbi. Shauri la askari lilikuwa kuwaua wafungwa, mtu asiogelee na kukimbia. Bali akida, akitaka kumponya Paulo, akawazuia, wasifanye kama walivyokusudia, akawaamuru wale wawezao kuogelea wajitupe kwanza baharini, wafike nchi kavu; nao waliosalia, hawa juu ya mbao na hawa juu ya vitu vingine vya merikebu. Na hivyo watu wote wakapata kuifikilia nchi kavu salama.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mdo 27:21-44