Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Dan 5:13-31

Dan 5:13-31 SUV

Ndipo Danieli akaletwa mbele ya mfalme. Na Mfalme akanena, akamwambia Danieli, Je! Wewe ndiwe Danieli yule, aliye mmoja wa wana wa Yuda waliohamishwa, ambao mfalme, baba yangu, aliwaleta huku toka Yerusalemu? Nimesikia habari zako, kwamba roho ya miungu imo ndani yako, na kwamba nuru na ufahamu na akili bora zimeonekana kwako. Basi sasa, watu wenye hekima na wachawi wameletwa mbele yangu, wapate kulisoma andiko hili, na kunijulisha tafsiri yake; lakini hawakuweza kunijulisha tafsiri ya jambo hili. Lakini nimesikia habari zako, kwamba waweza kuleta tafsiri, na kufumbua mafumbo; haya! Kama ukiweza kulisoma andiko hili, na kunijulisha tafsiri yake, utavikwa mavazi ya rangi ya zambarau, na kuwa na mkufu wa dhahabu shingoni mwako, nawe utakuwa mtu wa tatu katika ufalme. Ndipo Danieli akajibu, akasema mbele ya mfalme; Zawadi zako zishike wewe mwenyewe; na thawabu zako mpe mtu mwingine; walakini nitamsomea mfalme maandiko haya, na kumjulisha tafsiri yake. Kwa habari zako, Ee mfalme, Mungu Aliye juu alimpa Nebukadreza, baba yako, ufalme, na ukuu, na fahari, na utukufu; na kwa sababu ya ule ukuu aliompa, watu wa kabila zote, na mataifa, na lugha, wakatetemeka na kuogopa mbele yake; aliyetaka kumwua alimwua; na aliyetaka kumwacha hai, alimwacha hai; aliyetaka kumtukuza, alimtukuza; na aliyetaka kumshusha, alimshusha. Lakini moyo wake ulipoinuliwa, na roho yake ilipokuwa ngumu akatenda kwa kiburi, aliuzuliwa katika kiti chake cha enzi, nao wakamwondolea utukufu wake. Akafukuzwa mbali na wanadamu, moyo wake ukafanywa kuwa kama moyo wa mnyama, na makao yake yalikuwa pamoja na punda-mwitu; akalishwa majani kama ng’ombe, mwili wake ukalowa maji kwa umande wa mbinguni; hata alipojua ya kuwa Mungu Aliye juu ndiye anayetawala katika ufalme wa wanadamu, na ya kuwa humweka juu yake yeye amtakaye, awaye yote. Na wewe, mwanawe, Ee Belshaza, hukujinyenyekeza moyo wako, ijapokuwa ulijua hayo yote. Bali umejiinua juu ya Bwana wa mbingu; nao wamevileta vyombo vya nyumba yake mbele yako; na wewe, na wakuu wako, na wake zako, na masuria wako, mmevinywea; nawe umeisifu miungu ya fedha na ya dhahabu na ya shaba, na ya chuma, na ya mti, na ya mawe; wasioona, wala kusikia, wala kujua neno lo lote; na Mungu yule, ambaye pumzi yako i mkononi mwake, na njia zako zote ni zake, hukumtukuza. Ndipo kile kitanga cha ule mkono kikaletwa kutoka mbele zake, na maandiko haya yameandikwa. Na maandiko yaliyoandikwa ni haya; MENE, MENE, TEKELI, NA PERESI. Na tafsiri ya maneno haya ni hii; MENE, Mungu ameuhesabu ufalme wako na kuukomesha. TEKELI, umepimwa katika mizani nawe umeonekana kuwa umepunguka. PERESI, ufalme wako umegawanyika, nao wamepewa Wamedi na Waajemi. Ndipo Belshaza akatoa amri, nao wakamvika Danieli mavazi ya rangi ya zambarau, wakatia mkufu wa dhahabu shingoni mwake, wakapiga mbiu kutangaza habari zake, ya kwamba yeye ni mtu wa tatu katika ufalme. Usiku uo huo Belshaza, mfalme wa Wakaldayo, akauawa. Na Dario, Mmedi, akaupokea ufalme, naye umri wake alikuwa na miaka sitini na miwili.