Kut 9:13-26
Kut 9:13-26 SUV
BWANA akamwambia Musa, Ondoka asubuhi na mapema, ukasimame mbele ya Farao, umwambie, BWANA, Mungu wa Waebrania, asema, Wape watu wangu ruhusa waende ili wanitumikie. Kwani wakati huu nitaleta mapigo yangu yote juu ya moyo wako, na juu ya watumishi wako, na juu ya watu wako; ili upate kujua ya kuwa hapana mmoja mfano wa mimi ulimwenguni mwote. Kwa kuwa wakati huu ningekwisha kuunyosha mkono wangu, na kukupiga wewe na watu wako, kwa tauni, nawe ungekatiliwa mbali na kuondolewa katika nchi; lakini, nilikusimamisha wewe kwa sababu hii hii, ili nikuonyeshe uweza wangu, tena kwamba jina langu litangazwe katika dunia yote. Nawe, je! Hata sasa wajitukuza juu ya watu wangu, usiwape ruhusa waende zao? Tazama, kesho wakati kama huu, nitanyesha mvua ya mawe nzito sana, ambayo mfano wake haujakuwa huko Misri tangu siku ile ilipoanza kuwa hata hivi sasa. Basi sasa tuma wahimize waingie ndani wanyama wako na hayo yote uliyo nayo mashambani; kwani kila mtu na kila mnyama apatikanaye mashambani, wasioletwa nyumbani, hiyo mvua ya mawe itanyesha juu yao, nao watakufa. Yeye aliyelicha neno la BWANA miongoni mwa watumishi wa Farao aliwakimbiza watumishi wake na wanyama wake waingie nyumbani; na yeye asiyelitia moyoni neno la BWANA akawaacha watumishi wake na wanyama wake mashambani. BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako kuelekea mbinguni, ili iwe mvua ya mawe katika nchi yote ya Misri, juu ya wanadamu na juu ya wanyama, na juu ya mboga zote za mashamba, katika nchi yote ya Misri. Musa akaunyosha mkono wake kuelekea mbinguni; na BWANA akaleta ngurumo na mvua ya mawe, na moto ukashuka juu ya nchi; BWANA akanyesha mvua ya mawe juu ya nchi yote ya Misri. Basi palikuwa na mvua ya mawe, na moto uliochanganyikana na ile mvua ya mawe, nzito sana, ambayo mfano wake haukuwapo katika nchi yote ya Misri tangu ilipoanza kuwa taifa. Na ile mvua ya mawe ikapiga kila kilichokuwako mashambani, binadamu na mnyama, katika nchi yote ya Misri; hiyo mvua ya mawe ikapiga kila mmea wa mashambani, na kuuvunja kila mti wa mashamba. Katika nchi ya Gosheni peke yake, walikokaa wana wa Israeli, haikuwako mvua ya mawe.