Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwa 2:4-17

Mwa 2:4-17 SUV

Hivyo ndivyo vizazi vya mbingu na nchi zilipoumbwa. Siku ile BWANA Mungu alipoziumba mbingu na nchi hapakuwa na mche wa kondeni bado, wala mboga ya kondeni haijachipuka bado, kwa maana BWANA Mungu hajainyeshea nchi mvua, wala hapana mtu wa kuilima ardhi; ukungu ukapanda katika nchi, ukatia maji juu ya uso wote wa ardhi. BWANA Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai. BWANA Mungu akapanda bustani upande wa mashariki wa Edeni, akamweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya. BWANA Mungu akachipusha katika ardhi kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa; na mti wa uzima katikati ya bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya. Ukatoka mto katika Edeni wa kuitilia bustani maji, na kutokea hapo ukagawanyika kuwa vichwa vinne. Jina la wa kwanza ni Pishoni; ndio unaozunguka nchi yote ya Havila, ambako kuna dhahabu; na dhahabu ya nchi ile ni njema; huko kuna bedola, na vito shoham. Na jina la mto wa pili ni Gihoni; ndio unaozunguka nchi yote ya Kushi. Na jina la mto wa tatu ni Hidekeli; ndio unaopita mbele ya Ashuru. Na mto wa nne ni Frati. BWANA Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza. BWANA Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.