Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwa 9:8-17

Mwa 9:8-17 SUV

Mungu akamwambia Nuhu, na wanawe pamoja naye, akisema, Mimi, tazama, nalithibitisha agano langu nanyi; tena na uzao wenu baada yenu; tena na kila kiumbe hai kilichoko pamoja nanyi, ndege, na mnyama wa kufugwa, na kila mnyama wa mwitu katika nchi pamoja nanyi; wote wanaotoka katika safina, hata kila kilicho hai katika nchi. Na agano langu nitalithibitisha nanyi; wala kila chenye mwili hakitafutwa tena kwa maji ya gharika; wala hakutakuwa tena gharika, baada ya hayo, kuiharibu nchi. Mungu akasema, Hii ndiyo ishara ya agano nifanyalo kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai kilichoko pamoja nanyi, kwa vizazi vyote hata milele; Mimi nauweka upinde wangu winguni, nao utakuwa ni ishara ya agano kati yangu na nchi. Hata itakuwa nikitanda mawingu juu ya nchi, upinde utaonekana winguni, nami nitalikumbuka agano langu, lililoko kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai katika wote wenye mwili, wala maji hayatakuwa gharika tena kuwaharibu wote wenye mwili. Basi huo upinde utakuwa winguni; nami nitauangalia nipate kulikumbuka agano la milele lililoko kati ya Mungu na kila kiumbe hai katika wote wenye mwili kilichoko katika nchi. Mungu akamwambia Nuhu, Hii ndiyo ishara ya agano nililoliweka kati yangu na wote wenye mwili walioko katika nchi.