Yer 7:1-11
Yer 7:1-11 SUV
Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, kusema, Simama langoni pa nyumba ya BWANA, ukatangaze hapo neno hili, ukisema, Sikilizeni neno la BWANA, ninyi nyote wa Yuda, mnaoingia katika malango haya ili kumwabudu BWANA. BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tengenezeni njia zenu, na matendo yenu, nami nitawakalisha ninyi mahali hapa. Msitumainie maneno ya uongo, mkisema, Hekalu la BWANA, Hekalu la BWANA, Hekalu la BWANA ndiyo haya. Maana kama mkitengeneza kabisa njia zenu na matendo yenu; kama mkihukumu hukumu ya haki kati ya mtu na jirani yake; kama hamwonei mgeni, wala yatima, wala mjane, wala kumwaga damu isiyo na hatia mahali hapa, wala kuifuata miungu mingine kwa hasara yenu wenyewe; ndipo nitakapowakalisha mahali hapa, katika nchi hii niliyowapa baba zenu, tokea zamani hata milele. Angalieni, mnatumainia maneno ya uongo, yasiyoweza kufaidia. Je! Mtaiba, na kuua, na kuzini, na kuapa kwa uongo, na kumfukizia Baali uvumba, na kuifuata miungu mingine ambayo hamkuijua; kisha mtakuja na kusimama mbele zangu katika nyumba hii, iitwayo kwa jina langu, na kusema, Tumepona; ili mpate kufanya machukizo hayo yote? Je! Nyumba hii, iitwayo kwa jina langu, imekuwa pango la wanyang’anyi machoni penu? Angalieni, mimi, naam, mimi, nimeliona jambo hili, asema BWANA.