Yn 3:22-36
Yn 3:22-36 SUV
Baada ya hayo Yesu na wanafunzi wake walikwenda mpaka nchi ya Uyahudi; akashinda huko pamoja nao, akabatiza. Yohana naye alikuwa akibatiza huko Ainoni, karibu na Salimu, kwa sababu huko kulikuwa na maji tele; na watu wakamwendea, wakabatizwa. Maana Yohana alikuwa hajatiwa gerezani. Basi palitokea mashindano ya wanafunzi wa Yohana na Myahudi mmoja juu ya utakaso. Wakamwendea Yohana, wakamwambia, Rabi, yeye aliyekuwa pamoja nawe ng’ambo ya Yordani, yeye uliyemshuhudia, tazama, huyo anabatiza na watu wote wanamwendea. Yohana akajibu, akasema, Hawezi mtu kupokea neno lo lote isipokuwa amepewa kutoka mbinguni. Ninyi wenyewe mwanishuhudia ya kwamba nalisema, Mimi siye Kristo, bali nimetumwa mbele yake. Aliye naye bibi arusi ndiye bwana arusi; lakini rafiki yake bwana arusi, yeye anayesimama na kumsikia, aifurahia sana sauti yake bwana arusi. Basi hii furaha yangu imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua. Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote. Yeye aliye wa dunia, asili yake ni ya dunia, naye anena mambo ya duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni yu juu ya yote. Yale aliyoyaona na kuyasikia ndiyo anayoyashuhudia, wala hakuna anayeukubali ushuhuda wake. Yeye aliyeukubali ushuhuda wake ametia muhuri ya kwamba Mungu ni kweli. Kwa kuwa yeye aliyetumwa na Mungu huyanena maneno ya Mungu; kwa sababu hamtoi Roho kwa kipimo. Baba ampenda Mwana, naye amempa vyote mkononi mwake. Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu inamkalia.