Ayu 21
21
Ayubu Ajibu: Mwovu Hapatilizwi Daima
1Ndipo Ayubu akajibu, na kusema,
2Yasikizeni sana maneno yangu;
Jambo hili na liwe faraja yenu.
3Niacheni, nami pia nitanena;
Tena nikiisha nena, zidini kudhihaki.
4 #
1 Sam 1:16; Ayu 7:11,13; Zab 22:1-3 Mimi, je! Mashitaka yangu yamhusu mwanadamu?
Nami kwa nini nisikose kusubiri?
5Niangalieni, mkastaajabu,
Mkaweke mkono kinywani.
6Hata nikumbukapo nahuzunika,
Na utisho wanishika mwilini mwangu.
7 #
Ayu 12:6; Yer 12:1-3 Mbona waovu wanaishi,
Na kuwa wazee, naam, na kuongezeka kuwa na nguvu?
8Kizazi chao kinathibitika nao machoni pao,
Na wazao wao mbele ya macho yao.
9Nyumba zao zi salama pasina hofu,
Wala fimbo ya Mungu haiwapigi.
10Fahali wao huvyaza wala hapungukiwi na nguvu;
Ng’ombe wao mke huzaa, asiharibu mimba.
11Huwatoa kama kundi watoto wao.
Na watoto wao hucheza.
12Huimba kwa matari na kwa kinubi,
Na kuifurahia sauti ya filimbi.
13Siku zao hutumia katika kufanikiwa,
Kisha hushuka kuzimuni ghafula.
14Walakini walimwambia Mungu. Tuondokee;
Kwani hatutaki kuzijua njia zako.
15Huyo Mwenyezi ni nani, hata tumtumikie?
Nasi tutafaidiwa nini tukimwomba?
16Tazama, kufanikiwa kwao hakumo mkononi mwao;
Mashauri ya waovu na yawe mbali nami.
17Je! Ni mara ngapi taa yao waovu huzimishwa?
Na msiba wao kuwajilia?
Na Mungu kuwagawanyia uchungu kwa hasira yake?
18Ili wawe kama mabua makavu mbele ya upepo,
Kama makapi yaliyochukuliwa na dhoruba?
19Mwasema, Mungu huwawekea watoto wa mtu huo uovu wake.
Na amlipe mwenyewe, ili apate kuujua.
20Macho yake mwenyewe na yaone uharibifu wake,
Akanywe ghadhabu zake Mwenyezi.
21Kwani ana furaha gani katika mbari yake baada yake,
Hesabu ya miezi yake itakapokwisha katwa katikati?
22Je! Mtu awaye yote atamfundisha Mungu maarifa?
Naye ndiye awahukumuye walioko juu.
23Mmoja hufa katika nguvu zake kamili,
Mwenye kukaa salama na kustarehe;
24Vyombo vyake vimejaa maziwa,
Na mafuta ya mifupani mwake ni laini.
25Mwingine hufa katika uchungu wa roho,
Asionje mema kamwe.
26 #
Mhu 9:2; Isa 14:11 Wao hulala mavumbini sawasawa,
Mabuu huwafunika.
27Tazama, nayajua mawazo yenu,
Na mashauri mnayoazimia kwa uovu juu yangu.
28Kwa kuwa mwasema, Nyumba ya huyo mkuu i wapi?
Na hema waliyoikaa hao waovu i wapi?
29Je! Hamkuwauliza wapitao njiani?
Na maonyo yao hamyajui?
30 #
Mit 16:4; Nah 1:2 Kwamba mwovu huachiliwa katika siku ya msiba?
Na kuongozwa nje katika siku ya ghadhabu?
31Ni nani atakayetangaza njia yake usoni pake?
Tena ni nani atakayemlipa kwa hayo aliyofanya?
32Pamoja na hayo atachukuliwa kaburini,
Nao watalinda zamu juu ya ziara lake.
33 #
Ayu 3:17,18 Udongo wa bondeni utakuwa tamu kwake,
Na watu wote watafuata nyuma yake,
Kama vile walivyomtangulia watu wasiohesabika.
34Basi imekuwaje ninyi kunituza moyo bure,
Kwa kuwa katika jawabu zenu unasalia uongo tu.
Iliyochaguliwa sasa
Ayu 21: SUV
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.