Ayu 40:1-14
Ayu 40:1-14 SUV
BWANA akafuliza kumjibu Ayubu, na kusema, Je! Mwenye hoja atashindana na Mwenyezi? Mwenye kujadiliana na Mungu, na ajibu yeye. Ndipo Ayubu akamjibu Mungu, na kusema, Tazama, mimi si kitu kabisa, nikujibu nini? Naweka mkono wangu kinywani pangu. Nimenena mara moja, nami sitajibu; Naam, nimenena mara mbili, lakini sitaendelea zaidi. Ndipo BWANA akamjibu Ayubu katika upepo wa kisulisuli, na kusema, Jifunge viuno kama mwanamume, Mimi nitakuuliza neno, nawe niambie. Je! Hata hukumu yangu utaibatilisha? Utanitia mimi hatiani, upate kuhesabiwa haki? Au je! Wewe una mkono kama Mungu? Waweza kutoa ngurumo kwa sauti kama yeye? Haya! Jivike sasa fahari na ukuu; Jipambe heshima na enzi. Mwaga mafuriko ya hasira zako, Ukamtazame kila mtu mwenye kiburi, ukamdhili. Mtazame kila mtu mwenye kiburi ukamshushe, Ukawakanyage waovu hapo wasimamapo. Wafiche mavumbini pamoja, Wafunge nyuso zao mahali palipositirika. Ndipo mimi nami nitazikiri habari zako, Ya kuwa mkono wako wa kuume waweza kukuokoa.