Yoe 3:1-13
Yoe 3:1-13 SUV
Kwa maana, angalieni, siku zile, na wakati ule, nitakapowarudisha mateka wa Yuda na Yerusalemu, nitakusanya mataifa yote, nami nitawaleta chini katika bonde la Yehoshafau, na huko nitawahukumu kwa ajili ya watu wangu, na kwa ajili ya urithi wangu, Israeli, ambao wamewatawanya kati ya mataifa, na kuigawanya nchi yangu. Nao wamewapigia kura watu wangu; na mtoto mwanamume wamemtoa ili kupata kahaba, na mtoto mwanamke wamemwuza ili kupata divai, wapate kunywa. Naam, na ninyi ni kitu gani kwangu, enyi Tiro, na Sidoni, na nchi zote za Filisti? Je! Mtanirudishia malipo? Au mtanitenda neno lo lote? Upesi na kwa haraka nitawarudishia malipo yenu juu ya vichwa vyenu wenyewe. Kwa kuwa mmetwaa fedha yangu na dhahabu yangu, nanyi mmevichukua vitu vyangu vyema vipendezavyo, na kuviingiza katika hekalu zenu; tena watoto wa Yuda na watoto wa Yerusalemu mmewauzia Wayunani, mpate kuwahamisha mbali na mipaka yao; tazameni, nitawaamsha wapatoke mahali mlipowauza, nami nitawarudishia malipo yenu juu ya vichwa vyenu wenyewe. Na mimi nitawauza wana wenu na binti zenu, na kuwatia katika mikono ya wana wa Yuda, nao watawauzia watu wa Sheba, taifa lililo mbali kabisa; kwa maana BWANA ndiye aliyesema neno hili. Tangazeni haya kati ya mataifa; takaseni vita; waamsheni mashujaa; watu wa vita na wakaribie; na wapande juu. Yafueni majembe yenu yawe panga, na miundu yenu iwe mikuki; aliye dhaifu na aseme, Mimi ni hodari. Fanyeni haraka, mje, enyi mataifa yote, wa pande zote, jikusanyeni pamoja; na huko watelemshe mashujaa wako wote, Ee BWANA. Mataifa na wajihimize, wakapande juu katika bonde la Yehoshafau; maana huko ndiko nitakakoketi niwahukumu mataifa yote yaliyo pande zote. Haya! Utieni mundu, maana mavuno yameiva; njoni, kanyageni; kwa maana shinikizo limejaa, mapipa nayo yanafurika; kwani uovu wao ni mwingi sana.