Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mt 21:1-11

Mt 21:1-11 SUV

Hata walipokaribia Yerusalemu, na kufika Bethfage, katika mlima wa Mizeituni, ndipo Yesu alipotuma wanafunzi wawili akiwaambia, Enendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mara mtaona punda amefungwa, na mwana-punda pamoja naye; wafungueni mniletee. Na kama mtu akiwaambia neno, semeni, Bwana anawahitaji; na mara huyo atawapeleka. Haya yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema, Mwambieni binti Sayuni Tazama, mfalme wako anakuja kwako, Mpole, naye amepanda punda, Na mwana-punda, mtoto wa punda. Wale wanafunzi wakaenda zao, wakafanya kama Yesu alivyowaamuru, wakamleta yule punda na mwana-punda, wakaweka nguo zao juu yao, naye akaketi juu yake. Watu wengi katika ule mkutano wakatandaza nguo zao njiani; na wengine wakakata matawi ya miti, wakayatandaza njiani. Na makutano waliotangulia, na wale waliofuata, wakapaza sauti, wakisema, Hosana, Mwana wa Daudi; ndiye mbarikiwa, yeye ajaye kwa jina la Bwana; Hosana juu mbinguni. Hata alipoingia Yerusalemu, mji wote ukataharuki, watu wakisema, Ni nani huyu? Makutano wakasema, Huyu ni yule nabii, Yesu, wa Nazareti ya Galilaya.