Mk 12:13-27
Mk 12:13-27 SUV
Wakatuma kwake baadhi ya Mafarisayo na Maherodi, ili wamnase kwa maneno. Hata walipofika walimwambia, Mwalimu, twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, wala hujali cheo cha mtu; kwa maana hutazami sura za watu; lakini katika kweli waifundisha njia ya Mungu. Je! Ni halali kumpa Kaisari kodi au siyo? Tumpe, tusimpe? Naye, akijua unafiki wao, akawaambia, Mbona mmenijaribu? Nileteeni dinari niione. Wakaileta. Akawaambia, Ni ya nani sanamu hii na anwani hii? Wakamwambia, Ni ya Kaisari. Yesu akajibu, akawaambia, Mpeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na yaliyo ya Mungu mpeni Mungu. Wakamstaajabia sana. Kisha Masadukayo, watu wasemao ya kwamba hakuna kiyama, wakamwendea, wakamwuliza na kusema, Mwalimu, Musa alituandikia ya kwamba ndugu ya mtu akifa, akamwacha mkewe wala hana mtoto, ndugu yake amtwae yule mkewe akampatie ndugu yake mzao. Basi kulikuwa na ndugu saba, wa kwanza akatwaa mke, akafa, asiache mzao. Wa pili naye akamtwaa akafa, wala yeye hakuacha mzao. Na wa tatu kadhalika; hata na wote saba, wasiache mzao. Mwisho wa wote yule mwanamke akafa naye. Basi, katika kiyama atakuwa mke wa yupi katika hao? Maana wote saba walikuwa naye. Yesu akajibu, akawaambia, Je! Hampotei kwa sababu hii, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu? Kwa maana watakapofufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika walioko mbinguni. Na kwa habari ya wafu ya kwamba wafufuliwa, hamjasoma katika kitabu cha Musa, Sura ya Kijiti, jinsi Mungu alivyomwambia, akisema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo? Yeye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. Hivyo mwapotea sana.