Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mk 2:1-12

Mk 2:1-12 SUV

Akaingia Kapernaumu tena, baada ya siku kadha wa kadha, ikasikiwa ya kwamba yumo nyumbani. Wakakusanyika watu wengi, isibaki nafasi hata mlangoni; akawa akisema nao neno lake. Wakaja watu wakimletea mtu mwenye kupooza, anachukuliwa na watu wanne. Na walipokuwa hawawezi kumkaribia kwa sababu ya makutano, waliitoboa dari pale alipokuwapo; na wakiisha kuivunja wakalitelemsha godoro alilolilalia yule mwenye kupooza. Naye Yesu, alipoiona imani yao, akamwambia yule mwenye kupooza, Mwanangu, umesamehewa dhambi zako. Na baadhi ya waandishi walikuwako huko, wameketi, wakifikiri mioyoni mwao, Mbona huyu anasema hivi? Anakufuru. Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa mmoja, ndiye Mungu? Mara Yesu akafahamu rohoni mwake kwamba wanafikiri hivyo nafsini mwao, akawaambia, Mbona mnafikiri hivi mioyoni mwenu? Vyepesi ni vipi, kumwambia mwenye kupooza, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, ujitwike godoro lako, uende? Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (hapo amwambia yule mwenye kupooza), Nakuambia, Ondoka, ujitwike godoro lako uende nyumbani kwako. Mara akaondoka, akajitwika godoro lake, akatoka mbele yao wote; hata wakastaajabu wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Namna hii hatujapata kuiona kamwe.