Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zab 68:1-18

Zab 68:1-18 SUV

Mungu huondoka, adui zake wakatawanyika, Nao wamchukiao huukimbia uso wake. Kama moshi upeperushwavyo, Ndivyo uwapeperushavyo wao; Kama nta iyeyukavyo mbele ya moto, Ndivyo waovu wapoteavyo usoni pa Mungu. Bali wenye haki hufurahi, Na kuushangilia uso wa Mungu, Naam, hupiga kelele kwa furaha. Mwimbieni Mungu, lisifuni jina lake, Mtengenezeeni njia ya barabara, Apitaye majangwani kama mpanda farasi; Jina lake ni YAHU; shangilieni mbele zake. Baba wa yatima na mwamuzi wa wajane, Mungu katika kao lake takatifu. Mungu huwakalisha wapweke nyumbani; Huwatoa wafungwa wakae hali ya kufanikiwa; Bali wakaidi hukaa katika nchi kavu. Ee Mungu, ulipotoka mbele ya watu wako, Ulipopita nyikani, Nchi ilitetemeka Naam, mbingu zilidondoka usoni pa Mungu; Hata Sinai usoni pa Mungu; Mungu wa Israeli. Ee Mungu, ulinyesha mvua ya neema; Urithi wako ulipochoka uliutia nguvu. Kabila yako ilifanya kao lake huko; Ee Mungu, kwa wema wako uliwaruzuku walioonewa. Bwana analitoa neno lake; Wanawake watangazao habari ni jeshi kubwa; Wafalme wa majeshi wanakimbia, wanakimbia; Na mwanamke akaaye nyumbani agawa nyara. Kwa nini kulala mazizini arukapo hua, Mbawa zake ziking’aa kama fedha Na manyoya yake kama dhahabu? Mwenyezi Mungu alipotawanya wafalme huko, Kulinyesha theluji katika Salmoni. Ni mlima wa Mungu mlima Bashani, Ni mlima mrefu mlima Bashani. Enyi milima mirefu, kwani kuutazama kwa wivu Mlima alioutamani Mungu akae juu yake? Naam, BWANA atakaa juu yake milele. Magari ya Mungu ni ishirini elfu, maelfu maelfu; Bwana yumo kati yao kama katika Sinai, Katika patakatifu. Wewe umepaa juu, umeteka mateka, Umepewa vipawa katikati ya wanadamu; Naam, hata na wakaidi, BWANA Mungu akae nao.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Zab 68:1-18