1 Wafalme 6:1-18
1 Wafalme 6:1-18 SRUV
Ikawa katika mwaka wa mia nne na themanini baada ya wana wa Israeli kutoka nchini Misri, katika mwaka wa nne wa kutawala kwake Sulemani juu ya Israeli, katika mwezi wa Zivu, ndio mwezi wa pili, akaanza kuijenga nyumba ya BWANA. Nayo nyumba hiyo mfalme Sulemani aliyomjengea BWANA, urefu wake ulikuwa mikono sitini, na upana wake ishirini, na kwenda juu kwake mikono thelathini. Na ukumbi mbele ya hekalu la nyumba, urefu wake ulikuwa mikono ishirini, kadiri ya upana wa nyumba; na upana wake mikono kumi mbele ya nyumba. Akaifanyia nyumba madirisha ya miangaza yenye kimia. Nao ukuta wa nyumba akauzungushia vyumba, kushikamana na kuta za nyumba kotekote, za hekalu na za chumba cha ndani; akafanya vyumba vya mbavuni pande zote. Chumba cha chini kilikuwa mikono mitano upana wake, na chumba cha katikati kilikuwa mikono sita upana wake, na chumba cha tatu kilikuwa mikono saba upana wake; kwa kuwa upande wa nje akaupunguza ukuta wa nyumba pande zote, ili boriti zisishikamane kutani mwa nyumba. Na nyumba ilipokuwa ikijengwa, ikajengwa kwa mawe yaliyokwisha kuchongwa machimboni; wala nyundo, wala shoka, wala chombo cha chuma chochote, sauti yake haikusikiwa ilipokuwa ikijengwa nyumba. Mlango wa vyumba vya chini ulikuwapo upande wa kulia wa nyumba; mtu hupanda ngazi za kuzunguka mpaka vyumba vya katikati, na kutoka vile vya katikati mpaka vile vya tatu. Basi ndivyo alivyoijenga nyumba, akaimaliza; akaifunika nyumba kwa boriti na mbao za mwerezi. Akavijenga vyumba mbavuni mwa nyumba yote, kwenda juu kwake kila kimoja kilikuwa mikono mitano; vikaitegemea nyumba kwa boriti za mwerezi. Neno la BWANA likamjia Sulemani, kusema, Katika habari ya nyumba hii unayoijenga, kama ukienda katika sheria zangu, na kuzifanya hukumu zangu, na kuzishika amri zangu zote na kwenda katika hizo; ndipo nitakapolithibitisha neno langu kwako, nililomwambia Daudi baba yako. Nami nitakaa katikati ya wana wa Israeli, wala sitawaacha watu wangu Israeli. Basi Sulemani akaijenga hiyo nyumba akaimaliza. Akazijenga kuta za nyumba ndani kwa mbao za mwerezi; toka sakafu ya nyumba hata boriti za juu, akazifunika ndani kwa mti; akafunika sakafu ya nyumba kwa mbao za mberoshi. Akajenga mikono ishirini pande za nyuma za nyumba toka chini hata juu kwa mbao za mwerezi; naam, ndani akaijengea chumba cha ndani, yaani, patakatifu pa patakatifu. Nayo nyumba, ndiyo hekalu la mbele, ilikuwa mikono arubaini. Na ndani ya nyumba, mlikuwa na mwerezi ulionakishiwa maboga na maua yaliyofunuka wazi; mlikuwa na mwerezi mahali pote; wala mawe hayakuonekana.