Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 6:1-18

1 Wafalme 6:1-18 NENO

Katika mwaka wa mia nne na themanini baada ya Waisraeli kutoka nchi ya Misri, katika mwaka wa nne wa utawala wa Sulemani katika Israeli, katika mwezi wa Zivu, uliokuwa mwezi wa pili, alianza kujenga Hekalu la Mwenyezi Mungu. Hekalu ambalo Mfalme Sulemani alilijenga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu lilikuwa na urefu wa dhiraa sitini, upana wa dhiraa ishirini, na kimo cha dhiraa thelathini kwenda juu. Baraza iliyokuwa mbele ya ukumbi mkuu wa Hekalu iliongeza upana wa Hekalu kwa dhiraa ishirini, na kuchomoza dhiraa kumi mbele ya Hekalu. Akatengeneza madirisha membamba katika Hekalu. Akajenga vyumba vya pembeni kulizunguka Hekalu lote, vikishikamana na kuta za ukumbi wa Hekalu na za Patakatifu pa Patakatifu. Ghorofa ya chini kabisa ilikuwa na upana wa dhiraa tano, ya kati ilikuwa dhiraa sita, na ya tatu ilikuwa dhiraa saba. Kuzunguka ukuta wa nje wa Hekalu akapunguza ukuta pande zote ili boriti zisishikane kwenye kuta za Hekalu. Katika kujenga Hekalu, yalitumika tu mawe yaliyochongwa huko machimboni, wala hakuna nyundo, patasi au chombo kingine chochote cha chuma kilichosikika katika eneo la ujenzi wa Hekalu wakati lilipokuwa likijengwa. Ingilio la ghorofa ya chini kabisa lilikuwa upande wa kusini wa Hekalu; ngazi ilielekea ghorofa ya kati na kutoka hapo ilielekea hadi ghorofa ya tatu. Basi Sulemani akajenga Hekalu na kulikamilisha, akiliweka paa za boriti na mbao za mwerezi. Mfalme Sulemani akajenga vyumba vya pembeni kuzunguka Hekalu lote. Kimo cha kila kimoja kilikuwa dhiraa tano. Navyo vilikuwa vimeunganishwa na Hekalu kwa boriti za mwerezi. Neno la Mwenyezi Mungu likamjia Sulemani kusema: “Kuhusu Hekalu hili unalojenga, kama ukifuata amri zangu, ukatunza masharti yangu na kushika maagizo yangu yote na kuyatii, nitatimiza kupitia kwako ahadi niliyomwahidi Daudi baba yako. Nami nitakaa miongoni mwa Waisraeli, nami sitawaacha watu wangu Israeli.” Basi Sulemani akajenga Hekalu na kulikamilisha. Akazifunika kuta zake za ndani kwa mbao za mwerezi, akizipigilia ukutani kuanzia sakafuni mwa Hekalu hadi kwenye dari, na kufunika sakafu ya Hekalu kwa mbao za misunobari. Akagawa dhiraa ishirini sehemu ya nyuma ya Hekalu kwa mbao za mwerezi kuanzia kwenye sakafu hadi darini ili kufanya sehemu takatifu ya ndani, yaani Patakatifu pa Patakatifu. Ukumbi mkuu uliokuwa mbele ya chumba hiki ulikuwa na urefu wa dhiraa arobaini. Ndani, Hekalu lilipambwa na mbao za mwerezi zilizonakshiwa mifano ya maboga na maua yaliyochanua. Kila kitu kilikuwa cha mwerezi; hakuna jiwe ambalo lilionekana.