Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 6

6
Sulemani ajenga Hekalu
(2 Nyakati 3)
1Katika mwaka wa mia nne na themanini baada ya Waisraeli kutoka nchi ya Misri, katika mwaka wa nne wa utawala wa Sulemani katika Israeli, katika mwezi wa Zivu#6:1 mwezi wa tano katika kalenda ya Kiyahudi, uliokuwa mwezi wa pili, alianza kujenga Hekalu la Mwenyezi Mungu.
2Hekalu ambalo Mfalme Sulemani alilijenga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu lilikuwa na urefu wa dhiraa sitini#6:2 Dhiraa 60 ni sawa na mita 27., upana wa dhiraa ishirini#6:2 Dhiraa 20 ni sawa na mita 9., na kimo cha dhiraa thelathini#6:2 Dhiraa 30 ni sawa na mita 13.5. kwenda juu. 3Baraza iliyokuwa mbele ya ukumbi mkuu wa Hekalu iliongeza upana wa Hekalu kwa dhiraa ishirini, na kuchomoza dhiraa kumi mbele ya Hekalu. 4Akatengeneza madirisha membamba katika Hekalu. 5Akajenga vyumba vya pembeni kulizunguka Hekalu lote, vikishikamana na kuta za ukumbi wa Hekalu na za Patakatifu pa Patakatifu. 6Ghorofa ya chini kabisa ilikuwa na upana wa dhiraa tano#6:6 Dhiraa 5 ni sawa na mita 2.25., ya kati ilikuwa dhiraa sita#6:6 Dhiraa 6 ni sawa na mita 2.7., na ya tatu ilikuwa dhiraa saba#6:6 Dhiraa 7 ni sawa na mita 3.15.. Kuzunguka ukuta wa nje wa Hekalu akapunguza ukuta pande zote ili boriti zisishikane kwenye kuta za Hekalu.
7Katika kujenga Hekalu, yalitumika tu mawe yaliyochongwa huko machimboni, wala hakuna nyundo, patasi au chombo kingine chochote cha chuma kilichosikika katika eneo la ujenzi wa Hekalu wakati lilipokuwa likijengwa.
8Ingilio la ghorofa ya chini kabisa lilikuwa upande wa kusini wa Hekalu; ngazi ilielekea ghorofa ya kati na kutoka hapo ilielekea hadi ghorofa ya tatu. 9Basi Sulemani akajenga Hekalu na kulikamilisha, akiliweka paa za boriti na mbao za mwerezi. 10Mfalme Sulemani akajenga vyumba vya pembeni kuzunguka Hekalu lote. Kimo cha kila kimoja kilikuwa dhiraa tano. Navyo vilikuwa vimeunganishwa na Hekalu kwa boriti za mwerezi.
11Neno la Mwenyezi Mungu likamjia Sulemani kusema: 12“Kuhusu Hekalu hili unalojenga, kama ukifuata amri zangu, ukatunza masharti yangu na kushika maagizo yangu yote na kuyatii, nitatimiza kupitia kwako ahadi niliyomwahidi Daudi baba yako. 13Nami nitakaa miongoni mwa Waisraeli, nami sitawaacha watu wangu Israeli.”
14Basi Sulemani akajenga Hekalu na kulikamilisha. 15Akazifunika kuta zake za ndani kwa mbao za mwerezi, akizipigilia ukutani kuanzia sakafuni mwa Hekalu hadi kwenye dari, na kufunika sakafu ya Hekalu kwa mbao za misunobari. 16Akagawa dhiraa ishirini sehemu ya nyuma ya Hekalu kwa mbao za mwerezi kuanzia kwenye sakafu hadi darini ili kufanya sehemu takatifu ya ndani, yaani Patakatifu pa Patakatifu. 17Ukumbi mkuu uliokuwa mbele ya chumba hiki ulikuwa na urefu wa dhiraa arobaini#6:17 Dhiraa 40 ni sawa na mita 18.. 18Ndani, Hekalu lilipambwa na mbao za mwerezi zilizonakshiwa mifano ya maboga na maua yaliyochanua. Kila kitu kilikuwa cha mwerezi; hakuna jiwe ambalo lilionekana.
19Ndani ya Hekalu akatengeneza mahali patakatifu pa kuliweka Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu. 20Mahali patakatifu palikuwa na urefu wa dhiraa ishirini, upana wa dhiraa ishirini, na kimo cha dhiraa ishirini. Akapafunika upande wa ndani, na madhabahu ya mwerezi pia, kwa dhahabu safi. 21Sulemani akalifunika Hekalu upande wa ndani kwa dhahabu safi, na akaitandaza mikufu ya dhahabu kutoka upande mmoja hadi ule mwingine mbele ya mahali patakatifu, palipofunikwa kwa dhahabu. 22Basi akafunika upande wote wa ndani kwa dhahabu. Pia akafunika kwa dhahabu yale madhabahu yaliyokuwa ndani ya mahali patakatifu.
23Katika mahali patakatifu, akatengeneza makerubi wawili kwa mzeituni, kila moja likiwa na dhiraa kumi#6:23 Dhiraa 10 ni sawa na mita 4.5. kwenda juu. 24Bawa moja la kerubi wa kwanza lilikuwa na urefu wa dhiraa tano na bawa jingine dhiraa tano, hivyo urefu kutoka ncha ya bawa moja hadi ncha ya bawa jingine ulikuwa dhiraa kumi. 25Kerubi wa pili alikuwa na urefu wa dhiraa kumi pia, kwa kuwa makerubi hao wawili walifanana kwa vipimo na kwa umbo. 26Kimo cha kila kerubi kilikuwa dhiraa kumi. 27Aliwaweka makerubi hao katika chumba cha ndani kabisa cha Hekalu, mabawa yao yakiwa yamekunjuliwa. Bawa la kerubi mmoja liligusa ukuta mmoja, wakati bawa la yule mwingine liligusa ukuta wa upande mwingine, nayo mabawa yao mengine yaligusana katikati ya chumba. 28Akafunika wale makerubi kwa dhahabu.
29Kuta zote za Hekalu, za vyumba vya ndani na vya nje, zilipambwa kwa nakshi za makerubi, mitende na maua yaliyochanua. 30Pia alifunika sakafu zote za vyumba vya ndani na vya nje vya Hekalu kwa dhahabu.
31Katika ingilio la mahali patakatifu sana, alitengeneza milango ya mbao za mzeituni, yenye miimo ya sehemu moja ya tano ya upana wa madhabahu. 32Kwenye milango hiyo miwili ya mbao za mzeituni, alinakshi makerubi, mitende, pamoja na maua yaliyochanua, na kufunika makerubi na mitende kwa dhahabu iliyofuliwa. 33Kwa namna hiyo hiyo, alitengeneza miimo kwa mbao za mzeituni yenye upana wa robo ya upana wa ukumbi mkuu kwa ajili ya ingilio la ukumbi huo. 34Pia akatengeneza milango miwili kwa mbao za msunobari, kila mmoja ukiwa na vipande viwili ambavyo vilikunjwa kwa bawaba. 35Akanakshi makerubi, mitende na maua yaliyochanua juu yake, na kufunika kwa dhahabu iliyonyoshwa vizuri juu ya michoro.
36Tena akajenga ua wa ndani safu tatu za mawe yaliyochongwa, na safu moja ya boriti za mwerezi zilizosawazishwa.
37Msingi wa Hekalu la Mwenyezi Mungu uliwekwa katika mwaka wa nne, katika mwezi wa Zivu. 38Katika mwaka wa kumi na moja, mwezi wa Buli, ndio mwezi wa nane, Hekalu lilikamilika katika hatua zake zote kwa kufuatana na maelekezo yake Sulemani. Alilijenga kwa miaka saba.

Iliyochaguliwa sasa

1 Wafalme 6: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia