1 Wafalme 7
7
Sulemani ajenga jumba la kifalme
1Ilimchukua Sulemani miaka kumi na tatu kukamilisha ujenzi wa jumba lake la kifalme. 2Alijenga jumba lililoitwa Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni. Lilikuwa na urefu wa dhiraa mia moja#7:2 Dhiraa 100 ni sawa na mita 45., upana wa dhiraa hamsini#7:2 Dhiraa 50 ni sawa na mita 22.5., na kimo cha dhiraa thelathini#7:2 Dhiraa 30 ni sawa na mita 13.5., na safu nne za nguzo za mwerezi zilizoshikilia boriti za mwerezi zilizosawazishwa. 3Lilipauliwa kwa mbao za mwerezi juu ya boriti arobaini na tano zilizolalia nguzo, boriti kumi na tano kwa kila safu. 4Madirisha yake yaliwekwa juu kwa safu tatu, yakielekeana. 5Milango yenye miimo ya mstatili ilikuwa upande wa mbele katika safu tatu, ikielekeana.
6Akajenga safu ya nguzo, yenye urefu wa dhiraa hamsini#7:6 Dhiraa 50 ni sawa na mita 22.5. na upana wa dhiraa thelathini. Mbele ya jengo hilo kulikuwa na baraza. Mbele ya baraza kulikuwa na nguzo na paa lililoning’inia.
7Akajenga ukumbi wa kiti cha ufalme, yaani Ukumbi wa Hukumu, mahali ambapo angetolea hukumu, akaufunika kwa mbao za mwerezi kutoka sakafu hadi dari. 8Jumba la kifalme ambamo angeishi, aliliweka nyuma kidogo, na lilijengwa kama jumba hilo la hukumu. Pia Sulemani akajenga jumba la kifalme lililofanana na hilo kwa ajili ya binti Farao, aliyekuwa amemwoa.
9Majengo haya yote, kuanzia nje hadi kwenye ua mkuu, na kuanzia msingi hadi upenuni, yalijengwa kwa mawe yenye ubora wa hali ya juu, yaliyokatwa kwa vipimo kwa msumeno, na nyuso zake za ndani na za nje zililainishwa. 10Misingi ilijengwa kwa mawe makubwa yaliyo bora, yenye urefu wa dhiraa kumi#7:10 Dhiraa 10 ni sawa na mita 4.5., na mengine urefu wa dhiraa nane#7:10 Dhiraa nane ni sawa na mita 3.6.. 11Sehemu za juu kulikuwa na boriti za mwerezi, na mawe yenye ubora wa hali ya juu, yaliyokatwa kwa vipimo. 12Ule ua mkuu ulizungukwa na ukuta wa safu tatu za mawe yaliyochongwa, na safu moja ya boriti za mwerezi zilizosawazishwa, kama ulivyokuwa ua wa ndani wa Hekalu la Mwenyezi Mungu na baraza yake.
Samani za Hekalu
(2 Nyakati 4)
13Mfalme Sulemani akatuma watu Tiro kumleta Hiramu#7:13 au Huramu, 14ambaye mama yake alikuwa mjane kutoka kabila la Naftali na baba yake alikuwa mtu wa Tiro tena fundi wa shaba. Hiramu alikuwa na ustadi wa hali ya juu na mzoefu katika aina zote za kazi ya shaba. Alikuja kwa Mfalme Sulemani na kufanya kazi zake zote alizopangiwa.
15Hiramu akasubu nguzo mbili za shaba, kila moja ikiwa na urefu wa dhiraa kumi na nane#7:15 Dhiraa 18 ni sawa na mita 8.1., na mzingo wa dhiraa kumi na mbili#7:15 Dhiraa 12 ni sawa na mita 5.4. kwa mstari. 16Pia alitengeneza mataji mawili ya shaba ya kusubu ili kuyaweka juu ya hizo nguzo; kila taji lilikuwa na kimo cha dhiraa tano#7:16 Dhiraa 5 ni sawa na mita 2.25. kwenda juu. 17Wavu wa mikufu iliyosokotewa kwenye zile taji juu ya zile nguzo, saba kwa kila taji. 18Akatengeneza makomamanga katika safu mbili kuzunguka kila wavu kuremba mataji yaliyo juu ya nguzo. Alifanya hivyo kwa kila nguzo. 19Mataji yaliyokuwa juu ya nguzo kwenye baraza, yalikuwa katika umbo la yungiyungi, kimo chake ni dhiraa nne#7:19 Dhiraa nne ni sawa na mita 1.8.. 20Juu ya mataji ya zile nguzo mbili, juu ya ile sehemu yenye umbo kama bakuli, karibu na ule wavu, kulikuwa na yale makomamanga mia mbili katika safu kuzunguka pande zote. 21Hiramu akazisimamisha zile nguzo barazani pa Hekalu. Nguzo iliyokuwa upande wa kusini akaiita Yakini#7:21 maana yake Atathibitisha, na ile ya upande wa kaskazini akaiita Boazi#7:21 maana yake Imo nguvu. 22Mataji yaliyokuwa juu yalikuwa na umbo la yungiyungi. Hivyo kazi ya nguzo ikakamilika.
23Hiramu akasubu Bahari ya chuma, yenye umbo la mviringo, ya dhiraa kumi kutoka ukingo hadi ukingo, na kimo cha dhiraa tano. Mzunguko wake ulikuwa dhiraa thelathini. 24Chini ya ukingo, ilizungukwa na mapambo ya maboga kumi kwa kila dhiraa. Maboga hayo yalikuwa yamesubiwa katika safu mbili ili kuwa kitu kimoja na hiyo Bahari.
25Ile Bahari iliwekwa juu ya mafahali kumi na wawili, watatu wakielekea kaskazini, watatu wakielekea magharibi, watatu wakielekea kusini, na watatu wakielekea mashariki. Hiyo Bahari iliwekwa juu yao, na sehemu zao za nyuma zilielekeana. 26Bahari hiyo ilikuwa na unene wa nyanda moja#7:26 Nyanda moja ni sawa na sentimita 7.5., na ukingo wake ulifanana na ukingo wa kikombe, kama ua la yungiyungi lililochanua; nayo ingejazwa na bathi elfu mbili#7:26 Bathi 2,000 ni sawa na lita 40,000..
27Pia akatengeneza vitako kumi vya shaba vinavyoweza kuhamishika, kila kimoja kilikuwa na urefu wa dhiraa nne, upana dhiraa nne na kimo chake dhiraa tatu#7:27 Dhiraa 3 ni sawa na mita 1.35.. 28Hivi ndivyo vile vitako vilivyotengenezwa: Vilikuwa na mbao za pembeni zilizounganishwa na mihimili. 29Juu ya mbao kati ya hiyo mihimili kulikuwa na simba, mafahali na makerubi, pia kwenye mihimili yake. Juu na chini ya simba na mafahali kulikuwa na shada za maua yaliyofuliwa. 30Kila kitako kilikuwa na magurudumu manne ya shaba, na vyuma vya kuyazungusha. Kila kitako kilikuwa na sinia iliyowekwa juu ya vishikizo vinne viliyosubiwa shada za maua kila upande. 31Ndani ya kitako kulikuwa na nafasi ya wazi iliyokuwa na umbile la mviringo lenye kina cha dhiraa moja#7:31 Dhiraa moja ni sawa na sentimita 45.. Nafasi hii ya wazi ilikuwa ya mviringo, pamoja na kitako chake ilikuwa dhiraa moja na nusu#7:31 Dhiraa moja na nusu ni sawa na sentimita 67.5.. Kuzunguka huo mdomo wake kulitiwa nakshi. Papi za vitako zilikuwa mraba na si za mviringo. 32Yale magurudumu manne yalikuwa chini ya papi, na vyuma vya kuyazungushia viliunganishwa kwenye kitako. Kipenyo cha kila gurudumu kilikuwa dhiraa moja na nusu. 33Magurudumu hayo yalitengenezwa kama ya magari ya kukokotwa na farasi; vyuma vya kuzungushia magurudumu, duara zake, matindi yake na vitovu vyake, vyote vilikuwa vya kusubu.
34Kila kitako kilikuwa na mikono minne, moja kwenye kila pembe, ukichomoza kutoka kile kitako. 35Juu ya kitako kulikuwa na utepe wa mviringo wenye kina cha nusu dhiraa. Vishikio na papi vilishikamana upande wa juu wa kitako. 36Aliweka nakshi za makerubi, simba na mitende juu ya vishikio na juu ya papi, katika kila nafasi, na shada za maua kuzunguka. 37Hivi ndivyo Hiramu alivyotengeneza vile vitako kumi. Vyote vilisubiwa kwenye kalibu moja na vilifanana kwa vipimo na kwa umbo.
38Kisha akatengeneza masinia kumi ya shaba, kila moja likiwa na ujazo wa bathi arobaini#7:38 Bathi 40 ni sawa na lita 800., yakiwa na kipenyo cha dhiraa nne#7:38 Dhiraa nne ni sawa na mita 1.8. kila sinia moja kwa kila kimoja cha vile vitako kumi. 39Aliweka vitako vitano upande wa kusini wa Hekalu na vingine vitano upande wa kaskazini. Akaweka ile Bahari upande wa kusini, katika pembe ya kusini-mashariki ya Hekalu. 40Pia akatengeneza masinia, masepetu na mabakuli ya kunyunyizia.
Kwa hiyo Huramu akakamilisha kazi zote katika Hekalu la Mwenyezi Mungu kama vile Mfalme Sulemani alikuwa amemwagiza:
41nguzo mbili;
mataji mawili yenye umbo la bakuli juu ya hizo nguzo;
nyavu mbili za kupamba hayo mataji mawili yenye umbo la bakuli juu ya hizo nguzo;
42makomamanga mia nne kwa ajili ya hizo nyavu mbili (safu mbili za makomamanga kwa kila wavu, yakipamba hayo mataji mawili yenye umbo la bakuli juu ya hizo nguzo);
43vitako kumi pamoja na masinia yake kumi;
44ile Bahari ya chuma na wale mafahali kumi na wawili chini yake;
45masufuria, masepetu na mabakuli ya kunyunyizia.
Vyombo hivi vyote ambavyo Huramu alimtengenezea Mfalme Sulemani kwa ajili ya Hekalu la Mwenyezi Mungu vilikuwa vya shaba iliyong’arishwa. 46Mfalme akaamuru wavisubu katika kalibu ya udongo wa mfinyanzi katika uwanda wa Yordani ulio kati ya Sukothi na Sarethani. 47Sulemani hakupima vitu hivi vyote kwa sababu vilikuwa vingi sana; hivyo, uzani wa shaba haukukadiriwa.
48Sulemani pia akatengeneza samani zote zilizokuwa ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu:
madhabahu ya dhahabu;
meza ya dhahabu za kuweka mikate ya Wonesho;
49vinara vya taa vya dhahabu safi (vitano upande wa kuume na vitano upande wa kushoto, mbele ya mahali patakatifu);
shada za maua, na taa, na makoleo, vyote vikiwa vya dhahabu;
50vyombo vya dhahabu safi: masinia, mikasi ya kusawazishia tambi, mabakuli ya kunyunyizia, vyano na vyetezo;
na bawaba za dhahabu kwa ajili ya milango ya chumba cha ndani sana, yaani Patakatifu pa Patakatifu, na pia kwa ajili ya milango ya ukumbi mkuu wa Hekalu.
51Hivyo, Mfalme Sulemani alipomaliza kazi zote za Hekalu la Mwenyezi Mungu, akaviingiza ndani vile vitu ambavyo Daudi baba yake alikuwa ameviweka wakfu: fedha, dhahabu na samani; kisha akaviweka katika hazina za Hekalu la Mwenyezi Mungu.
Iliyochaguliwa sasa
1 Wafalme 7: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.