1 Wafalme 5
5
Maandalizi ya ujenzi wa Hekalu
(2 Nyakati 2:1-18)
1Hiramu mfalme wa Tiro aliposikia kuwa Sulemani amepakwa mafuta awe mfalme mahali pa Daudi baba yake, akatuma wajumbe kwa Sulemani, kwa sababu Hiramu siku zote alikuwa na uhusiano mzuri wa kirafiki na Daudi. 2Sulemani akapeleka ujumbe huu kwa Hiramu:
3“Unajua kwamba baba yangu Daudi hakuweza kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wake, kwa sababu ya vita vilivyopiganwa dhidi yake kutoka pande zote, hadi Mwenyezi Mungu alipowaweka adui zake chini ya miguu yake. 4Lakini sasa Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, amenipa utulivu kila upande hakuna adui wala maafa. 5Kwa hiyo, ninakusudia kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, kama Mwenyezi Mungu alivyomwambia baba yangu Daudi, aliposema, ‘Mwanao nitakayemweka kwenye kiti cha ufalme mahali pako, ndiye atajenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu.’
6“Hivyo toa amri ili mierezi ya Lebanoni ikatwe kwa ajili yangu. Watu wangu watafanya kazi na watu wako, nami nitakulipa kwa ajili ya watu wako kwa ujira wowote utakaoupanga. Unajua kwamba hatuna mtu yeyote mwenye ustadi katika kukata miti kama Wasidoni.”
7Hiramu aliposikia ujumbe wa Sulemani, akafurahishwa sana akasema, “Ahimidiwe Mwenyezi Mungu leo, kwa kuwa amempa Daudi mwana mwenye hekima ya kutawala taifa hili kubwa.”
8Hivyo Hiramu akapeleka ujumbe kwa Sulemani:
“Nimepokea ujumbe ulionipelekea na nitafanya yote unayohitaji katika kukupatia magogo ya mwerezi na misunobari. 9Watu wangu watayakokota kutoka Lebanoni hadi kwenye bahari, nami nitayafunga katika mafungu yaelee juu ya maji hadi utakapoelekeza. Huko nitayatenganisha, nawe utaweza kuyachukua. Wewe utakidhi haja yangu kwa kunipatia chakula kwa ajili ya watu wa nyumbani mwangu.”
10Kwa njia hii Hiramu akampa Sulemani miti yote ya mierezi na magogo ya misunobari kama alivyohitaji, 11naye Sulemani akampa Hiramu kori elfu ishirini#5:11 Kori 20,000 ni sawa na madebe 240,000. za ngano kama chakula kwa ajili ya watu wa nyumbani mwake, pamoja na mafuta safi ya zeituni yaliyokamuliwa bathi elfu ishirini#5:11 Bathi 20,000 ni sawa na madebe 200.. Sulemani aliendelea kumfanyia Hiramu hivyo mwaka baada ya mwaka. 12Mwenyezi Mungu akampa Sulemani hekima, kama alivyomwahidi. Palikuwa na uhusiano wa amani kati ya Hiramu na Sulemani, na wote wawili wakafanya mkataba.
13Mfalme Sulemani akakusanya wafanyakazi elfu thelathini kutoka Israeli yote. 14Akawapeleka Lebanoni kwa zamu za watu elfu kumi kila mwezi. Hivyo walikaa Lebanoni kwa mwezi mmoja, na miezi miwili wakakaa nyumbani. Adoniramu ndiye alikuwa kiongozi wa shokoa. 15Sulemani alikuwa na wachukuzi wa mizigo elfu sabini, na wachonga mawe elfu themanini huko vilimani, 16pamoja na wasimamizi elfu tatu mia tatu ambao walisimamia mradi huo na kuwaelekeza wafanyakazi. 17Kwa amri ya mfalme, walitoa mawe makubwa na bora kwenye machimbo ya mawe kwa kujengea msingi wa mawe yaliyochongwa kwa ajili ya Hekalu. 18Mafundi wa Sulemani, wa Hiramu na watu wa Gebali#5:18 yaani Bubilo walikata na kuandaa mbao na mawe kwa ajili ya ujenzi wa Hekalu.
Iliyochaguliwa sasa
1 Wafalme 5: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.