1 Wafalme 4
4
Maafisa na watawala wa Sulemani
1Basi Mfalme Sulemani akatawala Israeli yote.
2Hawa walikuwa maafisa wake wakuu:
Kuhani: Azaria mwana wa Sadoki;
3Elihorefu na Ahiya, wana wa Shisha: waandishi;
Yehoshafati mwana wa Ahiludi: karani;
4Benaya mwana wa Yehoyada: jemadari mkuu wa jeshi;
Sadoki na Abiathari: makuhani;
5Azaria mwana wa Nathani: kiongozi wa maafisa wa wilaya;
Zabudi mwana wa Nathani: kuhani na mshauri binafsi wa mfalme;
6Ahishari: msimamizi wa jumba la kifalme;
Adoniramu mwana wa Abda: msimamizi wa kazi za kulazimisha.
7Pia Sulemani alikuwa na watawala kumi na wawili wa wilaya katika Israeli yote, walioshughulikia mahitaji ya mfalme na ya watu wa nyumbani kwa mfalme. Kila mmoja alitoa chakula kwa mwezi mmoja katika mwaka.
8Majina yao ni haya:
Ben-Huri: katika nchi ya vilima ya Efraimu;
9Ben-Dekari: katika Makasi, Shaalbimu, Beth-Shemeshi na Elon-Beth-Hanani;
10Ben-Hesedi: katika Arubothi (Soko na nchi yote ya Heferi zilikuwa zake);
11Ben-Abinadabu: katika Nafoth-Dori (alimwoa Tafathi binti Sulemani);
12Baana mwana wa Ahiludi: katika Taanaki na Megido, na katika Beth-Shani yote karibu na Sarethani chini ya Yezreeli, kuanzia Beth-Shani hadi Abel-Mehola kupita hadi Yokmeamu;
13Ben-Geberi: katika Ramoth-Gileadi (makazi ya Yairi mwana wa Manase katika Gileadi ilikuwa yake, kadhalika wilaya ya Argobu katika Bashani na miji yake mikubwa sitini iliyozungukwa na kuta zenye makomeo ya shaba);
14Ahinadabu mwana wa Ido: katika Mahanaimu;
15Ahimaasi: katika Naftali (alikuwa amemwoa Basemathi binti Sulemani);
16Baana mwana wa Hushai: katika Asheri na katika Bealothi;
17Yehoshafati mwana wa Parua: katika Isakari;
18Shimei mwana wa Ela: katika Benyamini;
19Geberi mwana wa Uri: katika Gileadi (nchi ya Sihoni mfalme wa Waamori na nchi ya Ogu mfalme wa Bashani). Naye alikuwa mtawala pekee katika eneo hilo.
Mahitaji ya Sulemani ya kila siku
20Watu wa Yuda na Israeli walikuwa wengi kama mchanga wa pwani; walikula, wakanywa na kufurahi. 21Mfalme Sulemani akatawala katika falme zote kuanzia Mto#4:21 yaani Mto Frati hadi nchi ya Wafilisti, hadi kwenye mpaka wa Misri. Nchi hizi zilileta ushuru na zilikuwa chini ya Sulemani, siku zote za maisha yake.
22Mahitaji ya Sulemani ya kila siku yalikuwa kori thelathini#4:22 Kori 30 ni sawa na madebe 360. za unga laini, kori sitini#4:22 Kori 60 ni sawa na madebe 720. za unga wa kawaida. 23Ng’ombe kumi wa zizini, ng’ombe ishirini wa malisho, kondoo na mbuzi mia moja, pamoja na ayala, paa, kulungu na kuku wazuri sana. 24Kwa kuwa Sulemani alitawala falme zote magharibi ya Mto, kuanzia Tifsa hadi Gaza, naye akawa na amani pande zote. 25Wakati wa maisha ya Sulemani, watu wa Yuda na Israeli, kuanzia Dani hadi Beer-Sheba, waliishi salama, kila mtu chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake.
26Sulemani alikuwa na mabanda elfu nne#4:26 maandishi mengine yanasema elfu arobaini (taz. 2 Nyakati 9:25). ya magari ya vita, na farasi elfu kumi na mbili.
27Maafisa wa eneo hilo, kila mmoja katika mwezi wake, walileta mahitaji kwa ajili ya Mfalme Sulemani na wote waliokula mezani mwa mfalme. Walihakikisha kuwa hakuna chochote kilichopungua. 28Pia walileta kiasi walichopangiwa cha shayiri na majani kwa ajili ya farasi wa magari ya vita na farasi wengine mahali palipostahili.
Hekima ya Sulemani
29Mungu akampa Sulemani hekima na akili kubwa, pia ufahamu mpana usiopimika kama mchanga ulioko pwani ya bahari. 30Hekima ya Sulemani ilikuwa kubwa kuliko hekima ya watu wote wa Mashariki na kubwa kuliko hekima yote ya Misri. 31Alikuwa na hekima kuliko kila mwandishi, akiwemo Ethani Mwezrahi; kuliko Hemani, Kalkoli na Darda, wana wa Maholi. Umaarufu wake ukaenea kwa mataifa yote yaliyomzunguka. 32Akanena mithali elfu tatu, na nyimbo zake zilikuwa elfu moja na tano (1,005). 33Akaelezea maisha ya mimea kuanzia mwerezi wa Lebanoni hadi hisopo iotayo ukutani. Pia akafundisha kuhusu wanyama na ndege, wanyama wanaotambaa na samaki. 34Watu wa mataifa yote wakaja kusikiliza hekima ya Sulemani, wakiwa wametumwa na wafalme wote wa ulimwengu, waliokuwa wamesikia kuhusu hekima yake.
Iliyochaguliwa sasa
1 Wafalme 4: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.