Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 3

3
Sulemani aomba hekima
(2 Nyakati 1:3-12)
1Sulemani akafanya mapatano na Mfalme Farao wa Misri na akamwoa binti yake. Akamleta huyo binti Farao katika Mji wa Daudi hadi alipomaliza kujenga jumba lake la kifalme na Hekalu la Mwenyezi Mungu, pamoja na ukuta kuzunguka Yerusalemu. 2Hata hivyo, watu bado walikuwa wakitoa dhabihu huko kwenye mahali pa juu pa kuabudia, kwa sababu Hekalu lilikuwa bado halijajengwa kwa ajili ya Jina la Mwenyezi Mungu. 3Sulemani akaonesha upendo wake kwa Mwenyezi Mungu kwa kuenenda sawasawa na amri za Daudi baba yake, ila yeye alitoa dhabihu na kufukiza uvumba huko mahali pa juu pa kuabudia.
4Mfalme akaenda Gibeoni kutoa dhabihu, kwa maana ndipo palipokuwa mahali pa juu pa kuabudia pakuu, naye Sulemani akatoa sadaka elfu moja za kuteketezwa juu ya hayo madhabahu. 5Mwenyezi Mungu akamtokea Sulemani huko Gibeoni wakati wa usiku katika ndoto, naye Mungu akasema, “Omba lolote utakalo nikupe.”
6Sulemani akajibu, “Umemfanyia mtumishi wako, baba yangu Daudi, fadhili nyingi, kwa kuwa alikuwa mwaminifu kwako na mwenye haki, tena mnyofu wa moyo. Nawe umemzidishia fadhili hii kuu kwani umempa mwana wa kuketi kwenye kiti chake cha ufalme, kama ilivyo leo.
7“Sasa, Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, umemfanya mtumishi wako mfalme mahali pa baba yangu Daudi. Lakini mimi ni mtoto mdogo tu, wala sijui jinsi ya kutekeleza wajibu wangu. 8Mtumishi wako yuko hapa miongoni mwa watu uliowachagua: taifa kubwa, watu wengi wasioweza kuhesabika wala kutoa idadi yao. 9Hivyo mpe mtumishi wako moyo wa ufahamu ili kutawala watu wako na kupambanua kati ya mema na mabaya. Kwa maana, ni nani awezaye kutawala watu wako hawa walio wengi hivi?”
10Bwana akapendezwa kwamba Sulemani ameliomba jambo hili. 11Basi Mungu akamwambia, “Kwa kuwa umeomba neno hili na hukuomba maisha marefu au upate utajiri kwa nafsi yako, wala adui zako wafe, bali umeomba busara katika kutoa haki, 12nitafanya uliloomba. Nitakupa moyo wa hekima na wa ufahamu, kiasi kwamba hajakuwa mtu mwingine kama wewe, wala kamwe hatakuwa baada yako. 13Zaidi ya hayo, nitakupa yale ambayo hukuomba: utajiri na heshima; siku za maisha yako yote hapatakuwa na mtu kama wewe miongoni mwa wafalme. 14Nawe ukienenda katika njia zangu na kutii sheria na amri zangu vile baba yako Daudi alivyofanya, nitakupa maisha marefu.” 15Ndipo Sulemani akaamka, akatambua kuwa ilikuwa ndoto.
Akarudi Yerusalemu, akasimama mbele ya Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu, naye akatoa dhabihu za kuteketezwa na sadaka za amani. Kisha akawafanyia watumishi wake wote karamu.
Uamuzi wa hekima
16Basi wanawake wawili makahaba walikuja kwa mfalme na kusimama mbele yake. 17Mmoja wao akasema, “Bwana wangu, mimi na mwanamke huyu tunaishi kwenye nyumba moja. Nilikuwa nimezaa alipokuwa pamoja nami. 18Siku ya tatu baada ya mtoto wangu kuzaliwa, mwanamke huyu pia naye akazaa mtoto. Tulikuwa peke yetu, hapakuwa na mtu mwingine yeyote katika nyumba isipokuwa sisi wawili.
19“Usiku mwana wa huyu mwanamke akafa kwa sababu alimlalia. 20Hivyo akaondoka katikati ya usiku na kumchukua mwanangu kutoka ubavuni pangu wakati mimi mtumishi wako nilipokuwa nimelala. Akamweka kifuani mwake na kumweka mwanawe aliyekufa kifuani mwangu. 21Asubuhi yake, nikaamka ili kumnyonyesha mwanangu, naye alikuwa amekufa! Lakini nilipomwangalia kwa makini katika nuru ya asubuhi, niliona kuwa hakuwa yule mwana niliyemzaa.”
22Huyo mwanamke mwingine akasema, “Hapana! Mwana aliye hai ndiye wangu, aliyekufa ni wako.”
Lakini yule wa kwanza akasisitiza, “Hapana! Mwana aliyekufa ni wako; aliye hai ni wangu.” Hivi ndivyo walivyobishana mbele ya mfalme.
23Mfalme akasema, “Huyu anasema, ‘Mwanangu ndiye aliye hai, na aliyekufa ndiye mwanao,’ maadamu yule anasema, ‘Hapana! Aliyekufa ni wako, na aliye hai ni wangu.’ ”
24Kisha mfalme akasema, “Nileteeni upanga.” Basi wakamletea mfalme upanga. 25Ndipo mfalme akatoa amri: “Mkate mtoto aliye hai vipande viwili; mpe huyu nusu na mwingine nusu.”
26Mwanamke ambaye mwanawe alikuwa hai akajawa na huruma kwa ajili ya mwanawe na kumwambia mfalme, “Tafadhali, bwana wangu, mpe yeye mtoto aliye hai! Usimuue!”
Lakini yule mwanamke mwingine akasema, “Mkate vipande viwili. Asiwe wangu au wake!”
27Kisha mfalme akatoa uamuzi wake: “Mpeni mama wa kwanza mtoto aliye hai. Msimuue; ndiye mama yake.”
28Israeli yote iliposikia hukumu aliyotoa mfalme, wakamwogopa mfalme, kwa sababu waliona kuwa alikuwa na hekima kutoka kwa Mungu kwa kutoa haki.

Iliyochaguliwa sasa

1 Wafalme 3: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia