1 Samweli 1:7-20
1 Samweli 1:7-20 SRUV
Tena mumewe akafanya hivyo mwaka kwa mwaka, hapo yule mwanamke alipokwea kwenda nyumbani kwa BWANA, ndivyo yule alivyomchokoza; basi, kwa hiyo, yeye akalia, asile chakula. Elkana mumewe akamwambia, Hana, unalilia nini? Kwa nini huli? Kwa nini moyo wako una huzuni? Je! Mimi si bora kwako kuliko watoto kumi? Ndipo Hana akainuka, walipokula na kunywa huko Shilo. Naye Eli, kuhani, alikuwa akiketi kitini pake penye mwimo wa hekalu la BWANA. Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba BWANA akalia sana. Akaweka nadhiri, akasema, Ee BWANA wa majeshi, ikiwa wewe utayaangalia mateso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto wa kiume, ndipo mimi nitakapompa BWANA huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikia kichwani kamwe. Ikawa, hapo alipoendelea kuomba mbele za BWANA, Eli akamwangalia kinywa chake. Basi Hana alikuwa akinena moyoni mwake; midomo yake tu ilionekana kama anena, sauti yake isisikiwe; kwa hiyo huyo Eli alimdhania kuwa amelewa. Ndipo Eli akamwambia, Je! Utakuwa mlevi hadi lini? Achilia mbali divai yako. Hana akajibu, akasema, Hasha! Bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye roho ya huzuni, mimi sikunywa divai wala kileo, ila nimeimimina roho yangu mbele za BWANA. Usimdhanie mjakazi wako kuwa ni mwanamke asiyefaa kitu; kwa kuwa katika wingi wa kuugua kwangu na kusikitika kwangu ndivyo nilivyonena hata sasa. Ndipo Eli akajibu, akasema, Nenda kwa amani; na Mungu wa Israeli akujalie haja yako uliyomwomba. Naye akasema, Mjakazi wako na aone kibali machoni pako. Basi huyo mwanamke akaenda zake, naye akala chakula, wala uso wake haukuhuzunika tena. Wakaondoka asubuhi na mapema, wakaomba mbele za BWANA, kisha wakarejea na kufika nyumbani kwao huko Rama; Elkana akamjua mkewe Hana; naye BWANA akamkumbuka. Ikawa, wakati ulipowadia, Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto wa kiume; akamwita Samweli, akisema, Kwa kuwa nimemwomba kwa BWANA.