1 Samueli 1:7-20
1 Samueli 1:7-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Mambo haya yaliendelea mwaka baada ya mwaka. Kila mara Hana alipokwenda kwenye nyumba ya Mwenyezi-Mungu, Penina alimkasirisha Hana hata ikawa Hana analia na kukataa kula chochote. Elkana, mumewe, kila mara alimwuliza, “Kwa nini unalia? Kwa nini hutaki kula? Kwa nini una huzuni moyoni mwako? Je, mimi si bora kwako kuliko watoto kumi wa kiume?” Siku moja, walipokuwa wamemaliza kula na kunywa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu huko Shilo, Hana akasimama. Wakati huo, kuhani Eli alikuwa amekaa kwenye kiti karibu na mwimo wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Hana alikuwa na huzuni sana. Na alipokuwa anamwomba Mwenyezi-Mungu akawa analia kwa uchungu. Akaweka nadhiri akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi, kama tu utayaangalia mateso yangu mimi mtumishi wako ukanikumbuka mimi, bila kunisahau, mimi mtumishi wako, ukanijalia mimi mtumishi wako, mtoto wa kiume, nitakupa wewe Mwenyezi-Mungu mtoto huyo awe wako maisha yake yote; wembe hautapita kichwani pake kamwe.” Hana aliendelea kumwomba Mwenyezi-Mungu kwa muda mrefu, na kuhani Eli akawa anaangalia midomo yake. Hana alikuwa akiomba kimoyomoyo, lakini midomo yake ilikuwa inachezacheza, ila sauti yake haikusikika. Hivyo Eli akafikiri kuwa Hana amelewa. Kwa hiyo Eli akamwambia, “Utaendelea kulewa hadi lini? Achana na kunywa divai.” Lakini Hana akamjibu, “Sivyo bwana wangu; mimi ni mwanamke mwenye taabu mno; mimi sijanywa divai wala kinywaji kikali, bali nimekuwa nikimtolea Mwenyezi-Mungu yaliyomo rohoni mwangu. Usinidhanie kuwa mimi ni mwanamke asiyefaa kitu. Kwa muda wote huu nimekuwa nikisema mahangaiko yangu na taabu yangu.” Ndipo Eli akamwambia, “Nenda kwa amani; naye Mungu wa Israeli akupe kile ulichomwomba.” Hana akasema, “Naomba nami mtumishi wako nipate kibali mbele yako.” Hana akaenda zake, akala chakula na hakuwa na huzuni tena. Kesho yake asubuhi, Elkana na jamaa yake waliamka asubuhi na mapema, na baada ya kumwabudu Mwenyezi-Mungu, walirudi nyumbani Rama. Elkana akalala na mkewe Hana, naye Mwenyezi-Mungu akamkumbuka. Hivyo Hana akapata mimba, akajifungua mtoto wa kiume. Hana akamwita mtoto huyo Samueli, kwani alisema, “Nimemwomba kwa Mwenyezi-Mungu.”
1 Samueli 1:7-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Tena mumewe akafanya hivyo mwaka kwa mwaka, hapo yule mwanamke alipokwea kwenda nyumbani kwa BWANA, ndivyo yule alivyomchokoza; basi, kwa hiyo, yeye akalia, asile chakula. Elkana mumewe akamwambia, Hana, unalilia nini? Kwa nini huli? Kwa nini moyo wako una huzuni? Je! Mimi si bora kwako kuliko watoto kumi? Ndipo Hana akainuka, walipokula na kunywa huko Shilo. Naye Eli, kuhani, alikuwa akiketi kitini pake penye mwimo wa hekalu la BWANA. Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba BWANA akalia sana. Akaweka nadhiri, akasema, Ee BWANA wa majeshi, ikiwa wewe utayaangalia mateso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto wa kiume, ndipo mimi nitakapompa BWANA huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikia kichwani kamwe. Ikawa, hapo alipoendelea kuomba mbele za BWANA, Eli akamwangalia kinywa chake. Basi Hana alikuwa akinena moyoni mwake; midomo yake tu ilionekana kama anena, sauti yake isisikiwe; kwa hiyo huyo Eli alimdhania kuwa amelewa. Ndipo Eli akamwambia, Je! Utakuwa mlevi hadi lini? Achilia mbali divai yako. Hana akajibu, akasema, Hasha! Bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye roho ya huzuni, mimi sikunywa divai wala kileo, ila nimeimimina roho yangu mbele za BWANA. Usimdhanie mjakazi wako kuwa ni mwanamke asiyefaa kitu; kwa kuwa katika wingi wa kuugua kwangu na kusikitika kwangu ndivyo nilivyonena hata sasa. Ndipo Eli akajibu, akasema, Nenda kwa amani; na Mungu wa Israeli akujalie haja yako uliyomwomba. Naye akasema, Mjakazi wako na aone kibali machoni pako. Basi huyo mwanamke akaenda zake, naye akala chakula, wala uso wake haukuhuzunika tena. Wakaondoka asubuhi na mapema, wakaomba mbele za BWANA, kisha wakarejea na kufika nyumbani kwao huko Rama; Elkana akamjua mkewe Hana; naye BWANA akamkumbuka. Ikawa, wakati ulipowadia, Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto wa kiume; akamwita Samweli, akisema, Kwa kuwa nimemwomba kwa BWANA.
1 Samueli 1:7-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Tena mumewe akafanya hivyo mwaka kwa mwaka, hapo yule mwanamke alipokwea kwenda nyumbani kwa BWANA, ndivyo yule alivyomchokoza; basi, kwa hiyo, yeye akalia, asile chakula. Elkana mumewe akamwambia, Hana, unalilia nini? Kwani huli chakula? Kwa nini moyo wako una huzuni? Je! Mimi si bora kwako kuliko watoto kumi? Ndipo Hana akainuka, walipokwisha kula na kunywa huko Shilo. Naye Eli, kuhani, alikuwa akiketi kitini pake penye mwimo wa hekalu la BWANA. Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba BWANA akalia sana. Akaweka nadhiri, akasema, Ee BWANA wa majeshi, ikiwa wewe utaliangalia teso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto mume, ndipo mimi nitakapompa BWANA huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikilia kichwani kamwe. Ikawa, hapo alipodumu kuomba mbele za BWANA, Eli akamwangalia kinywa chake. Basi Hana alikuwa akinena moyoni mwake; midomo yake tu ilionekana kama anena, sauti yake isisikiwe; kwa hiyo huyo Eli alimdhania kuwa amelewa. Ndipo Eli akamwambia, Je! Utakuwa mlevi hata lini? Achilia mbali divai yako. Hana akajibu, akasema, Hasha! Bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye roho ya huzuni, mimi sikunywa divai wala kileo, ila nimeimimina roho yangu mbele za BWANA. Usimdhanie mjakazi wako kuwa ni mwanamke asiyefaa kitu; kwa kuwa katika wingi wa kuugua kwangu na kusikitika kwangu ndivyo nilivyonena hata sasa. Ndipo Eli akajibu, akasema, Enenda kwa amani; na Mungu wa Israeli akujalie haja yako uliyomwomba. Naye akasema, Mjakazi wako na aone kibali machoni pako. Basi huyo mwanamke akaenda zake, naye akala chakula, wala uso wake haukukunjamana tena. Wakaondoka asubuhi na mapema, wakasali mbele za BWANA, kisha wakarejea na kufika nyumbani kwao huko Rama; Elkana akamjua mkewe Hana; naye BWANA akamkumbuka. Ikawa, wakati ulipowadia, Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; akamwita jina lake Samweli, akisema, Kwa kuwa nimemwomba kwa BWANA.
1 Samueli 1:7-20 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hili liliendelea mwaka baada ya mwaka. Kila mara Hana alipokwenda katika nyumba ya BWANA, mke mwenzake alikuwa akimkasirisha mpaka analia na kushindwa kula. Elikana mumewe akawa anamwambia, “Hana, kwa nini unalia? Kwa nini huli? Kwa nini kuvunjika moyo? Je, mimi si bora zaidi kwako kuliko watoto kumi?” Siku moja walipokuwa wamemaliza kula na kunywa huko Shilo, Hana alisimama. Wakati huo kuhani Eli alikuwa ameketi kwenye kiti pembeni mwa mwimo wa mlango wa Hekalu la BWANA. Kwa uchungu wa rohoni Hana alilia sana na akamwomba BWANA. Naye akaweka nadhiri, akisema, “Ee BWANA Mwenye Nguvu Zote, laiti ungeangalia huzuni kuu ya mtumishi wako na kunikumbuka mimi, wala usimsahau mtumishi wako nawe ukampa mwana, basi huyo mwana nitamtoa kwa BWANA kwa siku zote za maisha yake, wala wembe hautapita kichwani mwake.” Alipokuwa anaendelea kumwomba BWANA, Eli alichunguza kinywa chake. Hana alikuwa akiomba moyoni mwake, midomo yake ikiwa inachezacheza lakini sauti haikusikika. Eli akafikiri alikuwa amelewa naye akamwambia, “Utaendelea kulewa mpaka lini? Achilia mbali mvinyo wako.” Hana akajibu, “Si hivyo bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye huzuni kubwa. Mimi sijanywa mvinyo wala kileo, nilikuwa ninaumimina moyo wangu kwa BWANA. Usimdhanie mtumishi wako kuwa mwanamke mwovu; nimekuwa nikiomba hapa katika wingi wa uchungu mkuu na huzuni.” Eli akamjibu, “Nenda kwa amani, naye Mungu wa Israeli na akujalie kile ulichomwomba.” Hana akasema, “Mtumishi wako na apate kibali machoni pako.” Kisha akaondoka zake na kula chakula, wala uso wake haukuwa na huzuni tena. Kesho yake asubuhi na mapema waliamka wakaabudu mbele za BWANA na kisha wakarudi nyumbani kwao huko Rama. Elikana akakutana kimwili na mkewe Hana, naye BWANA akamkumbuka. Hivyo wakati ulipotimia, Hana akapata mimba na akamzaa mwana. Hana akamwita jina lake Samweli, akasema, “Kwa kuwa nilimwomba kwa BWANA.”