2 Wakorintho 12:11-18
2 Wakorintho 12:11-18 SRUV
Nimekuwa mpumbavu, ninyi mmenilazimisha. Maana ilinipasa nisifiwe na ninyi; kwa sababu sikuwa duni ya mitume walio wakuu kwa lolote, nijapokuwa si kitu. Kweli ishara za mtume zilitendwa katikati yenu katika subira yote, kwa ishara na maajabu na miujiza. Maana ni kitu gani mlichopungukiwa kuliko makanisa mengine, ila kwa kuwa mimi sikuwalemea? Mnisamehe kosa hili. Tazama, hii ni mara ya tatu ya mimi kuwa tayari kuja kwenu, wala sitawalemea. Maana sivitafuti vitu vyenu, bali nawatafuta ninyi; maana haiwapasi watoto kuweka akiba kwa wazazi, bali wazazi kwa watoto. Nami nitakuwa radhi kutumia na kutumiwa kwa ajili yenu. Je! Kadiri nizidivyo kuwapenda sana, ninapungukiwa kupendwa? Lakini na iwe hivyo, mimi sikuwalemea; bali kwa kuwa mwerevu niliwapata kwa hila. Je! Mtu yeyote niliyemtuma kwenu, kwa mtu huyo niliwatoza kitu? Nilimwonya Tito, nikamtuma ndugu yule pamoja naye. Je! Tito aliwatoza kitu? Je! Hatukuenenda kwa Roho yeye yule na katika nyayo zile zile?