Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samweli 16

16
Adui za Daudi
1 # 2 Sam 9:9-10; 15:30; 9:2 Naye Daudi alipokipita punde hicho kilele cha mlima, tazama, Siba, mtumwa wa Mefiboshethi, akamkuta, na punda wawili waliotandikwa, na juu yao mikate mia mbili ya ngano, na vishada mia moja vya zabibu kavu, na matunda mia moja ya wakati wa joto, na kiriba cha divai. 2#Amu 5:10; 10:4; 2 Sam 15:1; 19:26; 1 Sam 25:27; 2 Sam 15:23; 17:29; Mit 31:6; Zab 104:15; 1 Tim 5:23 Mfalme akamwambia Siba, Ni za nini hizi? Siba akasema, Punda ni za jamaa ya mfalme wazipande; na mkate na matunda ni chakula cha hawa vijana; na divai ni kwamba wanywe hao wazimiao nyikani. 3#2 Sam 19:26-27 Mfalme akasema, Na mwana wa bwana wako yuko wapi? Siba akamwambia mfalme, Angalia, anakaa Yerusalemu; kwani alisema, Leo nyumba ya Israeli watanirudishia ufalme wa babu yangu. 4#2 Sam 14:10,11; Mit 18:13 Ndipo mfalme akamwambia Siba, Tazama, yote yaliyokuwa ni mali ya Mefiboshethi ni yako. Siba akasema, Mimi ninasujudu; na nione kibali machoni pako, Ee bwana wangu, mfalme.
Shimei amlaani Daudi
5 # 2 Sam 19:16; 1 Fal 2:8 Basi mfalme Daudi alipofika Bahurimu, tazama, kulitoka huko mtu wa jamaa ya nyumba ya Sauli, jina lake akiitwa Shimei, mwana wa Gera; alitoka, akalaani alipokuwa akienda. 6Tena akamtupia Daudi mawe, na watumishi wote wa mfalme Daudi; na watu wote na mashujaa wote walikuwako mkono wake wa kulia na mkono wake wa kushoto. 7Na Shimei alipolaani, alisema hivi, Nenda zako! Nenda zako! Ewe mtu wa damu! Ewe mtu usiyefaa! 8#Amu 9:24; 1 Fal 2:32,33; Ufu 16:6; 2 Sam 1:16; 3:28,29; 4:11,12 BWANA amerudisha juu yako damu yote ya nyumba ya Sauli ambaye umetawala badala yake; naye BWANA ametia ufalme katika mkono wa Absalomu mwanao; kisha, angalia, wewe umetwaliwa katika uovu wako mwenyewe, kwa sababu umekuwa mtu wa damu. 9#Kut 22:28 Ndipo Abishai mwana wa Seruya, akamwambia mfalme, Mbona mbwa mfu huyu amlaani mfalme bwana wangu? Na nivuke, nakusihi, nikaondoe kichwa chake. 10#2 Sam 3:39; 19:22; 1 Pet 2:23; 2 Fal 18:25; Omb 3:38; Rum 9:20 Mfalme akasema, Nina nini na ninyi, enyi wana wa Seruya? Kwa sababu yeye analaani, na kwa sababu BWANA amemwambia, Mlaani Daudi, basi, ni nani atakayesema, Mbona umetenda haya? 11Daudi akamwambia Abishai, na watumishi wake wote, Angalieni, huyu mwanangu, aliyetoka viunoni mwangu, anautafuta uhai wangu; sembuse Mbenyamini huyu? Mwacheni alaani, kwa sababu BWANA ndiye aliyemwagiza. 12#Mwa 29:32; 1 Sam 1:11; Zab 25:18; 37:7; Yer 24:5-7; Omb 3:22-26; Mt 5:11,12; Rum 8:28; 2 Kor 4:17 Labda BWANA atayaangalia mabaya yaliyonipata, naye BWANA atanilipa mema kwa sababu ya kunilaani kwake leo. 13Basi wakaendelea njiani Daudi na watu wake; Shimei naye akaaendelea juu ya ubavu wa kile kilima, kwa kumkabili, huku akiendelea, akilaani, akimtupia mawe, na kurusha mavumbi. 14Naye mfalme na watu wake wote waliokuwa pamoja naye wakafika, wakiwa wamechoka sana; naye akajiburudisha huko.
Ushauri wa Ahithofeli
15Absalomu, na hao watu wote wa Israeli, wakafika Yerusalemu, naye Ahithofeli alikuwa pamoja naye. 16Ikawa, Hushai, Mwarki, rafiki wa Daudi, alipomjia Absalomu, Hushai akamwambia Absalomu, Na aishi mfalme, aishi mfalme. 17#2 Sam 15:32,37; 19:25; Mit 17:17 Naye Absalomu akamwambia Hushai, Je! Huu ndio wema wako kwa rafiki yako? Mbona hukutoka pamoja na rafiki yako? 18Hushai akamwambia Absalomu, La, sivyo; lakini yule aliyechaguliwa na BWANA, na watu hawa, na watu wote wa Israeli, mimi nitakuwa wake, na pamoja naye nitakaa. 19#1 Sam 28:2; 2 Sam 15:34 Na tena, Ni nani ambaye yanipasa nimtumikie? Hainipasi kumtumikia mwanawe? Kama nilivyomtumikia baba yako, ndivyo nitakavyokuwa mbele yako.
20 # Kut 1:10; Zab 2:2; 37:12-15; Mit 21:30; Mt 27:1 Kisha Absalomu akamwambia Ahithofeli, Haya, toa ushauri wako, tufanyeje. 21#Mwa 35:22; 2 Sam 12:11; 15:16; Mwa 34:30; 1 Sam 13:4; 2 Sam 2:7; Zek 8:13; Law 18:8; 20:11; Kum 22:30; 27:20; Mit 28:7; Isa 3:9; Mik 7:3,6 Naye Ahithofeli akamwambia Absalomu, Ingia wewe kwa masuria wa baba yako, hao aliowaacha ili kutunza nyumba; na Israeli wote watasikia ya kuwa umechukizwa kabisa na baba yako; ndipo itatiwa nguvu mikono yao wote walio pamoja nawe. 22#2 Sam 12:11-12 Basi wakamtandikia Absalomu hema juu ya nyumba darini; naye Absalomu akaingia kwa masuria ya babaye machoni pa Israeli wote. 23#2 Sam 15:12 Na ushauri wake Ahithofeli, aliokuwa akiutoa siku zile, ulikuwa kama mtu aulizapo kwa neno la Mungu; ndivyo yalivyokuwa mashauri yote ya Ahithofeli, kwa Daudi, na kwa Absalomu.

Iliyochaguliwa sasa

2 Samweli 16: SRUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia