2 Timotheo 3:10-17
2 Timotheo 3:10-17 SRUV
Bali wewe umeyafuata mafundisho yangu, na mwenendo wangu, na makusudi yangu, na imani, na uvumilivu, na upendo, na subira; tena na adha zangu na mateso, mambo yaliyonipata katika Antiokia, katika Ikonio, na katika Listra, kila namna ya adha niliyoistahimili, naye Bwana aliniokoa katika hayo yote. Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa. Lakini watu waovu na wadanganyaji wataendelea, na kuzidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika. Bali wewe ukae katika mambo yale uliyofundishwa na kuhakikishwa, kwa maana unajua ni akina nani ambao ulijifunza kwao; na ya kuwa tangu utotoni umeyajua Maandiko Matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu. Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.