Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 26

26
Paulo ajitetea mbele ya Agripa
1Agripa akamwambia Paulo, Una ruhusa kusema maneno yako. Ndipo Paulo akanyosha mkono wake, akajitetea, 2Najiona nafsi yangu kuwa na heri, Ee mfalme Agripa, kwa kuwa nitajitetea mbele yako leo, katika mambo yale yote niliyoshitakiwa na Wayahudi. 3Hasa kwa sababu wewe unajua sana desturi na maswali yote waliyo nayo Wayahudi; kwa sababu hiyo nakuomba unisikilize kwa uvumilivu.
4Kwa maana Wayahudi wote wanajua maisha yangu tangu ujana, yalivyokuwa tangu mwanzo katika taifa langu huko Yerusalemu, 5#Mdo 23:6; Flp 3:5 wakinijua sana tangu mwanzo, kama wakipenda kushuhudia, ya kwamba nilikuwa Farisayo kwa kuifuata madhehebu ya dini yetu iliyo sahihi kabisa. 6#Mdo 28:20 Na sasa ninasimama hapa nihukumiwe kwa ajili ya tumaini la ahadi waliyopewa baba zetu na Mungu, 7#Mdo 24:15 ambayo kabila zetu kumi na mbili wanataraji kuifikia, wakimwabudu Mungu kwa bidii mchana na usiku. Nami ninashitakiwa na Wayahudi kwa ajili ya tumaini hilo, Ee Mfalme. 8Kwa nini limedhaniwa kwenu kuwa ni neno lisiloaminika, kwamba Mungu awafufua wafu? 9#Mdo 8:3; 22:4-5 Kweli, mimi mwenyewe niliona ndani ya nafsi yangu kwamba yanipasa kutenda mambo mengi yaliyopingana na jina lake Yesu Mnazareti; #Mdo 9:1-29; 22:3-21 10nami nikayafanya hayo Yerusalemu; niliwafunga wengi miongoni mwa watakatifu ndani ya magereza, nikiisha kupewa amri na wakuu wa makuhani; na walipouawa nilitoa idhini yangu. 11Na mara nyingi katika masinagogi yote niliwaadhibu, nikawashurutisha kukufuru; nikawaonea hasira kama mwenye wazimu, nikawaudhi hata katika miji ya ugenini.
Paulo asema juu ya kuongoka kwake
12Basi katika kazi hiyo nilipokuwa nikienda Dameski, mwenye mamlaka na maagizo ya wakuu wa makuhani; 13Ee Mfalme, ndipo wakati wa adhuhuri njiani niliona nuru inatoka mbinguni ipitayo mwangaza wa jua, ikinimulikia mimi, na wale waliofuatana nami pande zote. 14Tukaanguka nchi sote, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya Kiebrania, Sauli! Sauli! Mbona waniudhi? Ni vigumu kwako kuupiga mateke mchokoo. 15Nami nikasema, Wewe u nani, Bwana? Bwana akaniambia, Mimi ni Yesu, ambaye wewe unaniudhi. 16#Eze 2:1,3 Lakini inuka, usimame kwa miguu yako, maana nimekutokea kwa sababu hii, nikuweke wewe uwe mtumishi na shahidi wa mambo haya uliyoyaona, na wa mambo ambayo katika hayo nitajidhihirisha kwako; 17#Yer 1:7; 1 Nya 16:35 nikikuokoa na watu wako, na watu wa Mataifa, ambao nakutuma kwao; 18#Kum 33:3; Isa 35:5; 42:7,16; Mdo 20:32; Efe 2:2; Kol 1:13 uwafumbue macho yao, na kuwageuza waiache giza na kuielekea nuru, waziache na nguvu za Shetani na kumwelekea Mungu; kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi.
Paulo aeleza juu ya mahubiri yake
19 # Gal 1:16 Kwa hiyo, Ee Mfalme Agripa, sikuyaasi yale maono ya mbinguni, 20#Mdo 9:20,28-29; Mt 3:8 bali kwanza niliwahubiria wale wa Dameski na Yerusalemu, na katika nchi yote ya Yudea, na watu wa Mataifa, kwamba watubu na kumwelekea Mungu, wakiyatenda matendo yanayopatana na kutubu kwao. 21#Mdo 21:30,31 Kwa sababu ya hayo Wayahudi wakanikamata nikiwa ndani ya hekalu wakajaribu kuniua. 22#Lk 24:44-47 Basi kwa kuwa nimeupata msaada utokao kwa Mungu nimesimama hata leo hivi nikiwashuhudia wadogo kwa wakubwa, wala sisemi neno ila yale ambayo manabii na Musa waliyasema, kwamba yatakuwa; 23#Isa 42:6; 49:6; 1 Kor 15:20 ya kwamba Kristo hana budi kuteswa na ya kwamba yeye kwanza kwa kufufuliwa katika wafu atatangaza habari za nuru kwa watu wake na kwa watu wa Mataifa.
Paulo amwomba Agripa aamini
24Alipokuwa akijitetea hivi, Festo akasema kwa sauti kuu, Paulo, una wazimu, kusoma kwako kwingi kumekugeuza akili. 25Lakini Paulo akasema, Sina wazimu, Ee Festo mtukufu, bali nanena maneno ya kweli na ya akili kamili. 26#Yn 18:20 Kwa maana mfalme anajua habari za mambo haya, nami naweza kusema naye kwa ujasiri, kwa sababu najua sana ya kuwa hapana neno moja katika hayo asilolijua; kwa maana jambo hilo halikutendeka pembeni. 27Mfalme Agripa, je! Wawaamini manabii? Najua ya kuwa wawaamini. 28#Mdo 11:26; 1 Pet 4:16 Agripa akamwambia Paulo, Kwa maneno machache wadhani kunifanya mimi kuwa Mkristo. 29Paulo akamjibu, Namwomba Mungu kwamba, ikiwa kwa machache au ikiwa kwa mengi, si wewe tu ila na hao wote wanaonisikia leo wawe kama mimi, isipokuwa kuwa katika minyororo hii.
30Mfalme na mtawala na Bernike na wale walioketi pamoja nao wakasimama; 31hata walipoondoka wakasemezana, wakisema, Mtu huyu hatendi neno linalostahili kifo wala kufungwa. 32#Mdo 25:11 Agripa akamwambia Festo, Mtu huyo angeweza kufunguliwa, kama asingalitaka rufani kwa Kaisari.

Iliyochaguliwa sasa

Matendo 26: SRUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia