Kutoka 22:7-20
Kutoka 22:7-20 SRUV
Mtu akimpa mwenziwe amana ya fedha au vitu vingine amtunzie, na vitu vile vikaibwa katika nyumba ya mtu huyo; mwizi akipatikana, atalipa thamani yake mara mbili. Mwizi asipopatikana, ndipo mwenye nyumba atakaribia mbele ya Mungu, ionekane kwamba si yeye aliyetia mkono na kutwaa vyombo vya mwenziwe. Kila jambo la kukosana, kama ni la ng'ombe, au la punda, au la kondoo, au la mavazi, au la kitu chochote kilichopotea, ambacho mtu mmoja asema ni chake, hilo jambo la watu wote wawili litaletwa mbele ya Mungu; na yeye atakayehukumiwa na Mungu kuwa ni mkosa atamlipa mwenziwe thamani yake mara mbili. Mtu akimpa mwenziwe punda, au ng'ombe, au kondoo, au mnyama yeyote, ili amtunzie; yule mnyama akafa, au akaumia, au akachukuliwa mtu asione; patakuwa na kiapo cha BWANA katikati ya watu hao wawili, kwamba alipeleka mkono wake kutwaa mali ya mwenziwe, na mwenyewe atakubali hayo, wala hatalipa. Lakini kwamba aliibiwa mnyama huyo, sharti amlipe yule mwenyewe. Kama aliraruliwa na mnyama mkali, na amlete uwe ushahidi; hatalipa kwa ajili ya mnyama aliyeraruliwa. Mtu akiazima mnyama kwa mwenziwe, naye akaumia huyo mnyama, au akafa, mwenyewe asipokuwapo, lazima atalipa. Kama huyo mwenyewe alikuwapo pamoja na mnyama wake, hatalipa; kama ni mnyama wa kukodisha ni gharama ya kukodisha tu atakayepewa mwenyewe. Mtu akimshawishi mwanamwali, aliyeposwa na mume, na kulala naye, lazima atatoa mahari kwa ajili yake ili awe mkewe. Ikiwa baba yake huyo mwanamwali akataa kabisa kumpa, atalipa fedha kama hesabu ya mahari ya mwanamwali ilivyo. Usimwache mwanamke mchawi kuishi. Mtu yeyote alalaye na mnyama sharti atauawa. Mtu atakayemchinjia sadaka mungu yeyote, isipokuwa ni yeye BWANA peke yake, na angamizwe kabisa.