Kutoka 23:1-9
Kutoka 23:1-9 SRUV
Usivumishe habari za uongo; usishirikiane na mwovu kwa kuwa shahidi wa uongo. Usiwafuate walio wengi kutenda uovu; wala usitie ushahidi wako katika neno lolote kwa kugeukia kando na kuandamana na mkutano ili kupotoa hukumu; wala usimpendelee mtu mnyonge katika neno lake. Ukimwona ng'ombe wa adui wako, au punda wake, amepotea, sharti umrudishie mwenyewe tena. Ukimwona punda wake huyo akuchukiaye akiwa ameanguka chini ya mzigo wake, na wewe ungejizuia usimsaidie, lazima umsaidie. Usipotoe hukumu ya mtu maskini katika neno lake. Jitenge mbali na neno la uongo; wala wasio hatia na wenye haki usiwaue; kwa kuwa mimi sitamhesabia haki yeye aliye mwovu. Nawe usipokee rushwa; kwani hiyo rushwa huwapofusha macho hao waonao, na kuyapotoa maneno ya wenye haki. Usimwonee mgeni; maana, ninyi mwajua moyo wa mgeni ulivyo, kwa kuwa ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri.