Kutoka 23:1-9
Kutoka 23:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
“Usitoe habari za uongo. Usishirikiane na mtu mwovu ili kuwa shahidi mbaya. Usifuate genge la watu kutenda uovu, wala usijumuike na genge la watu kutoa ushahidi mahakamani ili kupotosha haki. Usiwe na upendeleo katika kesi ya maskini. “Ukimkuta ng'ombe au punda wa adui yako amepotea, utamrudishia mwenyewe. Ukimwona punda wa mtu anayekuchukia ameanguka na mzigo wake, msaidie mtu huyo kumsimamisha punda wake, wala usimwache na kwenda zako. “Usiipotoshe haki anayostahili maskini katika kesi yake. Jitenge mbali na mashtaka ya uongo wala usiwaue wasio na hatia na waadilifu, maana mimi sitamsamehe mtu mwovu. Usipokee rushwa, maana rushwa huwapofusha wakuu na kupotosha mambo ya wenye haki. “Usimdhulumu mgeni; nyinyi mwajua hali ya kuwa mgeni, maana mlikuwa wageni nchini Misri.
Kutoka 23:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Usivumishe habari za uongo; usishirikiane na mwovu kwa kuwa shahidi wa uongo. Usiwafuate walio wengi kutenda uovu; wala usitie ushahidi wako katika neno lolote kwa kugeukia kando na kuandamana na mkutano ili kupotoa hukumu; wala usimpendelee mtu mnyonge katika neno lake. Ukimwona ng'ombe wa adui wako, au punda wake, amepotea, sharti umrudishie mwenyewe tena. Ukimwona punda wake huyo akuchukiaye akiwa ameanguka chini ya mzigo wake, na wewe ungejizuia usimsaidie, lazima umsaidie. Usipotoe hukumu ya mtu maskini katika neno lake. Jitenge mbali na neno la uongo; wala wasio hatia na wenye haki usiwaue; kwa kuwa mimi sitamhesabia haki yeye aliye mwovu. Nawe usipokee rushwa; kwani hiyo rushwa huwapofusha macho hao waonao, na kuyapotoa maneno ya wenye haki. Usimwonee mgeni; maana, ninyi mwajua moyo wa mgeni ulivyo, kwa kuwa ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri.
Kutoka 23:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Usivumishe habari za uongo; usitie mkono wako pamoja na mwovu, kuwa shahidi wa udhalimu. Usiandamane na mkutano kutenda uovu; wala usitie ushahidi wako katika neno lo lote kwa kugeukia kando na kuandamana na mkutano ili kupotoa hukumu; wala usimpendelee mtu mnyonge katika neno lake. Ukimwona ng’ombe wa adui wako, au punda wake, amepotea, sharti umrudishie mwenyewe tena. Ukimwona punda wake huyo akuchukiaye hali ameanguka chini ya mzigo wake, nawe ungejizuia usimsaidie, lazima umsaidie. Usipotoe hukumu ya mtu maskini katika neno lake. Jitenge mbali na neno uongo; wala wasio hatia na wenye haki usiwaue; kwa kuwa mimi sitamhesabia haki yeye aliye mwovu. Nawe usipokee rushwa; kwani hiyo rushwa huwapofusha macho hao waonao, na kuyapotoa maneno ya wenye haki. Usimwonee mgeni; maana, ninyi mwajua moyo wa mgeni ulivyo, kwa kuwa ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri.
Kutoka 23:1-9 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
“Usieneze habari za uongo. Usimsaidie mtu mwovu kwa kuwa shahidi mwenye nia ya kudhuru wengine. “Usifuate umati wa watu katika kutenda mabaya. Unapotoa ushahidi kwenye mashtaka, usipotoshe haki ukijumuika na umati wa watu, nawe usimpendelee mtu maskini katika mashtaka yake. “Ukikutana na maksai au punda wa adui yako anapotea, hakikisha umemrudisha kwake. Ukiona punda wa mtu anayekuchukia ameanguka na mzigo wake, usimwache hapo alipoangukia; hakikisha kuwa umemsaidia. “Usiwanyime haki watu wako walio maskini katika mashtaka yao. Ujiepushe na mashtaka ya uongo, wala usimuue mtu asiye na hatia au mtu mwaminifu, kwa maana sitamhesabia hana hatia yeye aliye na hatia. “Usipokee rushwa, kwa kuwa rushwa hupofusha wale waonao, na kupinda maneno ya wenye haki. “Usimdhulumu mgeni; ninyi wenyewe mnajua jinsi mgeni anavyojisikia, kwa sababu mlikuwa wageni Misri.