Mwanzo 15:1-7
Mwanzo 15:1-7 SRUV
Baada ya mambo hayo neno la BWANA likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako itakuwa kubwa sana. Abramu akasema, Ee Bwana MUNGU, utanipa nini, nami naenda zangu hali sina mtoto, na atakayeimiliki nyumba yangu ni huyu Eliezeri, Mdameski? Abramu akasema, Tazama, hukunipa uzao, na mtumwa aliyezaliwa nyumbani mwangu ndiye mrithi wangu. Nalo neno la BWANA likamjia likinena, Huyu hatakurithi, bali utakayemzaa ndiye atakayekurithi. Akamtoa nje, akasema, Tazama juu mbinguni kisha uzihesabu nyota, kama unaweza kuzihesabu. Akamwambia, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako. Akamwamini BWANA, naye akamhesabia jambo hili kuwa haki. Kisha akamwambia, Mimi ni BWANA, niliyekuleta kutoka Uru wa Wakaldayo nikupe nchi hii ili uimiliki.