Mwanzo 18:16-33
Mwanzo 18:16-33 SRUV
Kisha watu hao wakaondoka huko wakaelekeza nyuso zao Sodoma. Abrahamu akaenda pamoja nao awasindikize. BWANA akasema, Je! Nimfiche Abrahamu jambo ambalo ninataka kulifanya, ikiwa Abrahamu atakuwa taifa kuu, hodari, na katika yeye mataifa yote ya dunia watabarikiwa? Kwa maana nimemchagua ili awaamuru wanawe na vizazi vyake baada yake wadumishe njia ya BWANA, kwa kuwa wenye haki na kweli, ili BWANA naye akamtimizie Abrahamu ahadi zake. BWANA akasema, Kwa kuwa kilio cha Sodoma na Gomora kimezidi, na dhambi zao zimeongezeka sana, basi, nitashuka sasa nione kama wanayotenda ni kiasi cha kilio kilichonijia; na kama sivyo, nitajua. Basi wale watu wakatoka huko wakaelekea Sodoma; lakini Abrahamu alibaki amesimama mbele za BWANA. Abrahamu akakaribia, akasema, Je! Utaharibu mwenye haki pamoja na mwovu? Huenda wakawapo wenye haki hamsini katika mji, utaharibu, wala hutauacha mji kwa ajili ya hao hamsini wenye haki waliomo? La hasha! Usifanye hivyo, ukamwue mwenye haki pamoja na mwovu, mwenye haki awe kama mwovu. Hasha! Mhukumu ulimwengu wote asitende haki? BWANA akasema, Nikiona katika Sodoma wenye haki hamsini mjini, nitapaacha mahali pote kwa ajili yao. Abrahamu akajibu, akasema, Basi, nimeshika kusema na Bwana, nami ni mavumbi na majivu tu. Huenda wakapunguka watano katika wale hamsini wenye haki, je! Utaharibu mji wote kwa kupungua watano? Akasema, Sitauharibu, nikiona humo arubaini na watano. Akazidi tena kusema naye, akinena, Huenda wakaonekana humo arubaini? Akasema, Sitafanya kwa ajili ya hao arubaini. Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema, Huenda wakaonekana huko thelathini? Akasema, Sitafanya, nikiona humo thelathini. Akasema, Tazama, nimeshika kusema na Bwana, huenda wakaonekana huko ishirini? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao ishirini. Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema mara hii tu, Huenda wakaonekana huko kumi? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao kumi. Basi BWANA alipokwisha kuzungumza na Abrahamu, akaenda zake; Abrahamu naye akarudi mahali pake.